Wakati kukiwa na gumzo mitaani kuhusu uhalali wa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza unaompa mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli ushindi wa asilimia 65, chama hicho kimedai kimepunguziwa ushindi.

Mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba amelalamika kuwa utafiti huo umewapunguzia ushindi kwa kuwa wanategemea ushindi mkubwa zaidi ya huo wa 65%.

Siku kadhaa zilizopita, Makamba alieleza kuwa chama hicho kilifanya utafiti kupitia kampuni ambayo hakuitaja na ulionesha mgombea urais wa chama hicho atashinda kwa asilimia 69.

Akiongea na gazeti la gazeti la Mwananchi, mjumbe huyo ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Bumbuli alisema kuwa chama chake hakishitushwi na utafiti huo kwa kuwa mgombea wao amefika zaidi vijijini kuliko wagombea wengine.

“CCM haishangazwi na matokeo hayo kwa sababu Magufuli amefika maeneo ya vijijini zaidi kuliko mgombea yeyote, ameleeleza sera zinazoeleweka na ana sifa za uadilifu lakini wanojadili mabadilio hawaendani na historia yao na ndio maana wananchi wamekatishwa tama na mienendo yao,” Makamba anakaririwa.

Hata hivyo, utafiti huo umepingwa na wasomi wengi wakiwemo wahadhiri na viongozi wa taasisi kubwa zinazojihusisha na kazi za jamii na tafiti.

Mkurugenzi wa taasisi ya SIKIKA, Inei Kiria, alipinga sampuli iliyotumika katika utafiti huo pamoja na njia ya kuwapata watu 1848 waliohojiwa, ambao alisisitiza hawatoshi kuwakilisha idadi ya wapiga kura takribani milioni 24 nchi nzima.

Kadhalika, Professa Gaudencia Mpangalla wa Chuo Kikuu Cha Ruaha alieleza kuwa na shaka na methodolojia iliyotumiwa na Twaweza kupata majibu hayo kwa kuwa hayatoi picha halisi ya hali ya kisiasa nchini kwa wakati huu.

Kauli iliyoungwa mkono na mwenyekiti wa mitandao ya mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Arusha, Petro Ahham, “Kwa hali ilivyo sasa huwezi kusema kuna mshindi wa asilimia 65, babda watueleze walioulizwa maswali ni waliojiandikisha tu na sio hawa tunaowaona kwenye mikutano.”

Wasomi wengine waliohojiwa walieleza kuwa na shaka na watu waliohojiwa kwa kuwa inaonesha kuwa walipewa simu na chaja, hali inayoweza kupelekea majibu kuwa na mlengo fulani wa ushawishi wa vitu hivyo walivyopewa.

Roma Apokea Ofa Kibao Kushuti Video Ya ‘Viva’
Eva Carneiro Aondoka Stamford Bridge