Mgombea ubunge wa jimbo la Bunda mjini kwa tiketi ya Chadema, Ester Bulaya juzi alimuokoa mtoto wa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Stephen Wasira aliyekuwa anataka kuchomwa moto na wananchi.

Kwa mujibu wa Ester Bulaya, mtoto huyo aliyetajwa kwa jina la Kambarage alitaka kuchomwa moto katika kata ya Kunzugu eneo la Bukore kwa madai ya kukamatwa na wananchi hao akigawa rushwa kwa baadhi ya vijana ili waweze kufanya fujo kwenye mkutano wa mgombea huo uliopangwa kufanyika katika eneo hilo hivi karibuni.

Akiongea na waandishi wa habari jana, Bi. Bulaya amesema kuwa alipata taarifa kuwa wananchi wamewafungia ndani ya nyumba makada kadhaa wa CCM akiwemo mtoto wa Wasira na aliamua kuwachukua askari wa jeshi la polisi na kuwahi katika eneo la tukio ambapo waliwakuta watu hao.

“Jana (Juzi) mtoto wa Wasira na wenzake tumewaokoa wakitaka kuchomwa moto ndani na wananchi ambao walipata taarifa zao za kukutana ili wawape watu rushwa waje kufanya fujo kwenye mkutano wangu ninaopanga kuufanya Bukore,” alieleza Ester Bulaya.

Mgombea huyo alivitaka vyombo vya usalama na wagombea kwa pamoja kukemea vitendo hivyo vya rushwa vinavyoweza kupelekea uvunjifu wa amani.

Kwa upande wa Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Bunda, Alex Mpenda alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa alifika kwenye eneo la tukio na kukuta watu hao wameshaondolewa na jeshi la polisi.

Maalim Seif, Lowassa Kuirudisha Katiba Ya Warioba
Stephane Henchoz Ampiga Dongo Shaqiri