Aliyekua kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Fabio Capello amepasua ukweli wa kusuasua kwa klabu bingwa nchini humo Chelsea, ambayo imeshindwa kuonyesha mwanzo mzuri msimu huu.

Capello ambaye aliachana na timu ya taifa ya Urusi Julai 14 mwaka huu, amesema kuanza vibaya kwa klabu hiyo ya jijini London kumetokana na mazoea ya meneja wao Jose Mourinho ambayo yamekua yakimgharimu mara kwa mara.

Capello, amesema Mourinho hakuwandaa vyema wachezaji wake katika hali ya kupambana wakati wote na badala yake aliamini msimu huu, huenda ungekua na sura sawa na ule uliopita ambao ulimalizika kwa Chelsea kutwaa ubingwa.

Amesema anashangazwa na baadhi ya watu kuwanyooshea vidole wachezaji wa The Blues, kwa kuwatuhumu wamekua hawajitumi, lakini kwake analiona tatizo lipo kwa mkuu wa kikosi hicho.

Capello, amekumbushia hali kama hiyo iliwahi kutokea, wakati Mourinho akiwa na kikosi cha klabu ya Real Madrid, ambapo baada ya kutwaa ubingwa wa nchini Hispania msimu wa 2011–12, alibweteka na msimu uliofuata hakufanya vyema na ndio ukawa mwisho wake huko Estadio Stantiago Bernabeu.

Kutokana na maelezi hayo, Capello ametoa angalizo kwa mashabiki pamoja na viongozi wa klabu ya Chelsea, kuwa na mtazamo chanya kwa Jose Mourinho, kwani anachokifanya kwa sasa hakistahili kuendelezwa zaidi ya kubadili mbinu za upambanaji.

Mpaka sasa Chelsea wameshapoteza michezo minne ya ligi ya nchini England, wameshinda miwili na kutoka sare mara mbili, hali ambayo imeifanya klabu hiyo ya magharibi mwa jijini London, kusalia katika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi kwa kumiliki point nane.

Zawadi Ya Khanga Ya 'Kijani' Yazua Tafrani kwenye ‘Kitchen Party’
Nasri: Hata Baba Yangu Akiwa Kocha Sirudi