Kiungo wa klabu ya Man City, Samir Nasri ameapa kutotengua maamuzi yake, ya kutoichezea tena timu ya taifa ya Ufaransa, ambayo inatarajia kuwa mwenyeji wa fainali za mataifa ya Ulaya za mwaka 2016.

Nasri alitangaza kuachana na timu ya taifa ya Ufaransa, baada ya kuachwa kenye kikosi kilichoitwa na kocha mkuu Didier Deschamps, kwa ajili ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2014 zilizofanyika nchini Brazil.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28, amesema haoni sababu ya kugeuza maamuzi aliyoyachukua na kuyatangaza hadharani, kutokana na azimio alilojiweka na kuhakikisha anajikita katika soka la upande wa klabu yake ya Man City.

Mbali na kuendelea na msimamo huo, kiungo huyo akaenda mbali zaidi kwa kusema hata kama baba yake mzazi atakua kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ufaransa siku za usoni, na akadiriki kumuita kikosini hatoitikia wito huo.

Samir Nasri aliachwa kwenye kikosi kilichoshiriki fainali za kombe la dunia za mwaka 2014, kwa kisingizio cha kutokua na nidhamu ya kutosha, na jambo hilo lilidhihiri wakati wa fainali za mataifa ya Ulaya za mwaka 2012 ambapo alionyesha kutoridhishwa na maamuzi ya kocha Laurent Blanc ya kumtoa uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na mchezaji mwingine.

Lakini pamoja na kutilia mkazo wa kucheza soka katika upande wa klabu, Samir Nasri bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kumridhisha meneja wa klabu ya Man City, Manuel Pellegrini baada ya kusajiliwa kwa Raheem Sterling pamoja na Kevin De Bruyne.

Kwa msimu huu, Nasri amepata bahati ya kutumika kwenye kikosi cha Man City, mara saba, na wakati mwingine amekua akiingia kama mchezaji wa akiba.

Fabio Capello: Tatizo Ni Mourinho Sio Wachezaji
Flora Mbasha na Mumewe, Mapenzi Kama Zamani