Baada ya kutikisa kibiriti juma lililopita kwa kusema huenda msimu huu ukawa wa mwisho kwake katika himaya ya Old Trafford, meneja wa Man Utd Jose Mourinho amemjibu kiungo Michael Carrick.

Kiungo huyo ambaye alionyesha kuchoshwa na mkakati wa Mourinho tangu alipotua klabuni hapo mwezi Julai mwaka huu, ameahidiwa mkataba mpya ambao utamuwezesha kuendelea kuwepo Old Trafford.

Mourinho amesema Carrick ni mtu wa kipekee katika kikosi chake, na wakati mwingine amekua akihitaji kumtumia katika michezo muhimu kama iliyokua mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Arsenal.

Amesema alishtushwa na msimamo wa Carrick alioutangaza kupitia kituo cha televisheni cha Sky Sports juma lililopita, na hakudhani kama angefikia hatua ya kuweka wazi mustakabali wa kutohitaji kuendelea kuwepo Man Utd.

“Ilinisikitisha sana niliposikia taarifa ile, na sijui ni kwa nini Carrick alifanya maamuzi magumu ya kuzungumza katika chombo cha habari, kwangu mimi ninamuamini na kuthamini mchango wake hapa (Old Trafford).

“Nimekua na mazungumzo naye mara kwa mara na wakati mwingine tunazungumza kuhusu mchezo wa soka, lakini hakuwahi kuniambia dukuduku lake kuhusu kuondoka, eti kwa kigezo cha kuchoshwa na mpango wa kutomtumia kwenye kikosi cha kwanza,”

“Ninamuhakikishia atasaini mkataba mpya, na atacheza katika kikosi cha Man Utd kama ilivyokua kwenye mpambano wa Arsenal ambapo alionyesha uwezo mkubwa.” Alisema Mourinho

Yaya Toure Kusajiliwa Ligi Ya Mabingwa Barani Ulaya
Zinedine Zidane: Ronaldo Amefunga Mjadala Wa Ballon d'Or