Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  alikuwa hajui kama yeye ni Mwenyekiti wa Baraza la Kudhibiti Dawa za Kulevya kama ilivyobainishwa kwenye sheria.
Ameyasema hayo wakati wa akiwaapisha viongozi mbalimbali, Ikulu na kuagiza wakachape kazi bila kumuogopa mtu yeyote.
“Kama anajua basi amejua jana au leo, nina uhakika hata Mawaziri wake ambao ni wajumbe wa baraza hilo walikuwa hawana taarifa na hakuna aliyewakumbusha, hata mimi sikuletewa mapendekezo ya kumteua Kamishna Mkuu wa Mamlaka hii ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga,”amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ameeleza kuchukizwa na kitendo cha watu kwenda Kituo Kikuu Polisi (Central) na kuanza kuosha gari la mtuhumiwa huku wengine wakienda na kwaya katika eneo hilo.
Tukio hilo lilitokea Alhamisi iliyopita wakati mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji alipokwenda kuripoti polisi na baadhi ya mashabiki wake kuosha gari lake lililokuwa limeegeshwa katika kituo hicho.
Wengine wanaoaminika kuwa ni wanakwaya wa Kanisa la Ufufuo na uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima walifika eneo hilo wakati kiongozi wao alipokwenda kuhojiwa huku wakiimba nyimbo mbalimbali.

Elimu yazidi kuporomoka visiwani Zanzibar
Magazeti ya Tanzania leo Februari 13, 2017