Saa chache baada ya Rais John Magufuli kutangaza kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, kigogo huyo amepinga tuhuma zilizopelekea kusimamishwa kwake akidai kuwa hana hatia.

Rais Magufuli alitangaza jana kumsimamisha kazi Kabwe baada ya kusikiliza maelezo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyedai kuwa Tume aliyoiunda umebaini kuwa alifanya udanganyifu na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 3.

Kabwe amemueleza mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi kuwa anasubiri uchunguzi ufanyike kama alivyoelekeza Rais Magufuli ambao utabainisha ukweli huku akihoji kama atalipwa fidia endapo atabainika hakuhusika.

“Nimekwambia sina la kukwambia kwa sasa lakini nasema tu kwamba sina shida na hilo, uchunguzi utafanyika na nina uhakika ukweli utajulikana tu,” alisema Kabwe. “Lakini kama ikibainika kuwa nimeonewa, Je, kuna fidia yoyote nitalipwa,” alihoji.

Awali, Kabwe alisema kuwa maelezo aliyoyatoa Makonda kuhusu utata wa mikataba aliyoisaini na wazabuni iliyodaiwa kuwa na udanganyifu wa kukwepa sheria na taratibu zilizoinyima serikali mapato, Kabwe alisema kuwa hayo ni maoni binafsi ya Makonda kwani hakuna utata wowote kwenye mikataba husika.

Mrema kutinga Dar kudai ahadi yake kwa Rais Magufuli
Hospitali yageuka duka la watoto, yauza vichanga kwa bei hii