Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro, amewataka wananchi kuondoa hofu na kuendelea na shughuli zao za kawaida kwani jeshi hilo liko imara na hakuna atakayeandamana Septemba 1.

Chadema wametangaza Septemba 1 kuwa siku maalum ya kufanya maandamano na mikutano nchi nzima kwa kile walichodai ni kupinga kuminywa kwa demokrasia nchini kupitia operesheni waliyoipa jina la UKUTA.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda Sirro alisema kuwa Jeshi hilo liko imara kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayethubutu kuingia barabarani kuandamana.

“Habari ya Ukuta haipo, umeshabomoka na kama haujabomoka utabomoka, wakazi wa Dar es Salaam msiwe na hofu, fanyeni kazi na hata siku hiyo hakuna mtu atakayejitokeza barabarani kuandamana,” alisema Kamanda Sirro.

Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro alieleza kuwa jeshi hilo limekamata fulana zenye ujumbe wa kichochezi katika duka moja lililoko maeneo ya Kinondoni pamoja na kumtia nguvuni muuzaji aliyetajwa kwa jina la Yoram Sethy Mbyellah.

Fulana hizo zilikuwa na maandishi yanayouna mkono oparesheni Ukuta yakisomeka “TUJIPANGE TUKATAE UDIKITETA UCHWARA’’  “UKUTA”

Jeshi hilo limewataka wananchi kuhakikisha wanatii sheria bila shuruti na kwamba wanaotaka kufanya fujo ama uvunjifu wa amani watambue kuwa kwa Dar es Salaam nafasi hiyo haipo.

Waliokula fedha za Chama cha ushirika kuchukuliwa hatua, Katavi
Lowassa: Chadema ni nani hadi tukapambane na Polisi..?