Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete amesema kuwa nchi za Ulaya zina jukumu la kihistoria la kuzisaidia nchi za Afrika na kwamba waafrika hawawezi kuikwepa misaada hiyo.

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili unaojadili malengo mapya 17 ya Umoja wa Mataifa yanayohusu ‘Maendeleo Endelevu kwa mwaka 2030’, Dk. Kikwete alisema kuwa nchi za Ulaya zinajukumu hilo kwa kuwa uchumi wake umetokana na rasilimali walizovuna kutoka Afrika wakati wa Ukoloni.

Hata hivyo, Dk. Kikwete alifafanua kuwa misaada hiyo sio lazima iwe ya kifedha bali hata uwekezaji katika viwanda kwa kuzingatia sheria inayowalinda na kuwafaidisha zaidi wazawa.

“Misaada tunayoizungumzia siyo lazima iwe fedha, bali tunahitaji wawekeze zaidi kwetu kwa mikataba ya kisheria inayolinda wazawa, kwa mfano Tanzania tuna rasilimali za kutosha kama gesi, madini na vinginevyo, lakini hivi vyote vinahitaji kuibuliwa na kutayarishwa. Lazima tuwape nafasi ili kufanikisha lakini kwa sheria zitakazowalinda Watanzania,” Dk. Kikwete anakaririwa.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli aliwataka watanzania kufanya kazi kwa bidii na kuinua uchumi wa nchi ili waondokane na misaada aliyoiita ‘mkate wa masimango’ kutoka kwa wahisani.

Rais Magufuli alisema kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi na kwamba haipaswi kuwa ombaomba bali inapaswa kuwa nchi inayotoa misaada kwa nchi nyingine (donor country).

Kauli hiyo ya Rais Magufuli ilikuja siku chache baada ya Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la Marekani kutangaza kusitisha msaada wa takribani shilingi trilioni moja kwa Tanzania kutokana na kutoridishwa na uamuzi wa uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar na namna Sheria ya Makosa ya Mtandao ilivyotekelezwa.

Manji Na Makamu Wake, Clement Sanga Kuchukua Fomu Leo
Hukumu ya Mafisadi itakayotolewa na mahakama ya Mafisadi yawekwa wazi