Kiongozi wa mbio maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu Luteni Josephine Mwambashi amekataa kufungua mradi wa Zahanati ya Mrao Keryo iliyopo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro baada ya kubaini matumizi mabaya ya fedha wakati wa ujenzi huo.
Luteni Mwambashi amefikia uamuzi huo baada ya kufanya uchunguzi wa kupitia nyaraka za ujenzi wa mradi, na kubaini kiasi cha shilingi milioni 100 kutoonekana matumizi yake kati ya shilingi milioni 204.8 zilizotolewa.
Aidha ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo kufanya uchunguzi wa fedha zaidi ya shilingi milioni 100 ambazo hazionekani matumizi yake katika ujenzi wa zahanati.
Rais Karia asema alivyoisaidia Young Africans
Amesema hajaridhishwa na nyaraka zilizopo, kwani zinaonesha Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) imechangia shilingi milioni 163.7 huku ikionesha gharama za ujenzi ni shilingi milioni 111.814 hadi mradi kukamilika, zikitofautiana na gharama za ujenzi za halmashauri ambazo ni shilingi milioni 204.8.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo Mary Robert amesema kuwa ujenzi huo ulianza Oktoba 16 mwaka 2013, ambapo kwa sasa wananchi zaidi ya mia mbili wanapata huduma katika zahanati hiyo ya Mrao Keryo.