Baada ya kupoteza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons mwishoni mwa juma lililopita, Kocha Mkuu wa Namungo FC Denis Kitambi, amesema matokeo ya mchezo huo yamemshangaza kutokana na wachezaji wake kucheza tofauti.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Jumamosi (Machi 11) kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi, Namungo wakiwa nyumbani walifungwa mabao 2-3 dhidi ya Tanzania Prisons.

Kitambi amesema walikuwa na mpango wa kushinda mchezo huo, lakini hakuelewa namna wachezaji wake walivyocheza kipindi cha kwanza.

“Kipindi cha kwanza kwetu hakikuwa bora na hatukuelewa namna ilivyokuwa, kila muda tulikuwa tunafanyia kazi makosa yetu ili kupata ushindi, lakini ikashindikana.”

“Tulikuwa tunarekebisha makosa kwenye mapigo huru, wachezaji wanafanya makosa tena, unarekebisha hilo wanarudia, hiyo haikuwa nzuri kwetu.”

“Ambacho tunakifanya kwa sasa ni kufanyia kazi makosa ili kupata matokeo mazuri kwenye mechi zijazo,” amesema Kitambi.

Kichapo hicho kimeiacha Namungo FC ikiwa na alama 32 zinazoiweka nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Tanzania Prisons ikifikisha alama 25 ikiwa nafasi ya 14.

Chalamila aitaka TAKUKURU kuchunguza mradi Kituo cha Maroli
Brahim Diaz ampagawisha meneja AC Milan