Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa amewakumbusha Wabunge na Mameya wa chama hicho ambao watashindwa kutekeleza vizuri majukumu yao kuwa watafukuzwa katika chama hicho.

Ikumbukwe kuwa kitendo cha kutimuliwa uanachama kinaweza kupelekea mbunge au Meya kupoteza nafasi yake moja kwa moja.

Lowassa alikumbusha tahadhari hiyo jana alipokutana na Mameya na Manaibu Meya wa Ukawa walioshinda katika Manispaa za Kinondoni na Ilala jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza kwa vyama vya upinzani kushika nafasi hiyo tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Waziri Mkuu huyo wa zamani aliwapongeza viongozi hao wapya na kuwataka kufanya kazi kubwa ili kuwaonesha wananchi kuwa hawakukosea kuchagua Ukawa na waone tofauti ya maendeleo kati ya vyama hivyo vya upinzani na CCM.

“Hili ni agizo la Kamati Kuu (Chadema) kwamba mbunge na hata Meya wakishindwa ku-perform, ikipita mwaka mmoja au miwili hawajafanya chochote watafukuzwa kwenye chama,” alisema Lowassa.

Aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanafanya kazi kubwa ya kuliweka jiji la Dar es Salaam kuwa safi na kutatua matatizo ya usafiri kwa wananchi.

Kadhalika, aliwataka viongozi hao kukusanya mapato kuliko wakati mwingine wowote. Pia, kutoogopa kukopa katika mabenki ili waanzishe miradi endelevu itakayowagusa wananchi moja kwa moja.

Mwanasiasa huyo mkongwe pia aliwataka Mameya na Manaibu Meya hao kuhakikisha wanakubaliana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwa hawataingiliwa na kuzuiwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya katika kutekeleza majukumu yao.

“Muondokane na sheria inayowazuia kukopa benki, kopeni benki na chagueni miradi ambayo inawagusa wananchi,” Lowassa alieleza.

Kwa upande wa Mameya na Manaibu Meya hao, walimshukuru Lowassa kwa jinsi alivyowasaidia kushinda ikiwa ni pamoja na kuwatia moyo na kuwajenga kusaikolojia.

“Lowassa alituandaa kama timu, alituweka kambini na kutujenga kisaikolojia. Kambi hii ndio chachu ya ushindi wetu,” Meya wa Ilala, Charles Kuyeko wa Chadema, tamko liloungwa mkono na Naibu Meya wa Kinondoni, Jumanne Amir wa CUF.

Mtoto wa Kikwete ahusishwa Kuuziwa UDA kwa bei yaKutupwa, kukwepa kodi
Djokovic Ajitetea Tuhuma Za Kupanga Matokeo