Mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli jana alizua taharuki jukwaani alipokuwa anawahutubia wananchi wa Shinyanga, baada ya kuchanganya majina na kumtaja kada aliyekuwa amekaa jukwaa kuu kama mmoja kati ya wasaliti wa chama hicho.

Magufuli ambaye aliamua kutaja majina ya watu aliodai kuwa wanafanya kazi mchana kama watiifu kwa CCM lakini usiku wanafanya kazi ya kumsaidia mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

“Kuna baadhi ya wana CCM wanatuhujumu sana, wengine tunajua hata majina. Bahati nzuri mimi huwa sisemi uongo, kuna huyu Gasper, mchana tunakuwa naye CCM lakini usiku anaungana na wapinzani,” Magufuli ananukuliwa.

Baada ya kutaja jina hilo, Gasper ambaye alikuwa jukwaani alionekana kuwa na taharuki huku umati uliohudhuria pia ukiwa katika taharuki. Hata hivyo, mjumbe wa kamati ya kampeni ya chama hicho, Abdallah Bulembo alilazimika kumfuata Magufuli na kumnong’oneza.

Baada ya kupata ufafanuzi, mgombea huyo alifanya masahihisho kwenye jina hilo na kueleza kuwa aliyekuwa anamzungumzia sio Gasper aliyeko jukwani (Gasper Kileo), na aliyemtaja kama msaliti ni Gasper Antony.

Gasper Antony alipata nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo na kukiri kuwa alikuwa anamuunga mkono Lowassa alipokuwa CCM lakini baada ya kujiunga na Chadema hivi sasa hamuungi mkono, bali anamuunga mkono Magufuli.

Lowassa Atangaza Mbinu Mpya Ya Kupambana Na Rushwa
Kumekucha: Lowassa, Magufuli Waanza Kutajana