Na Josefly Muhozi:

Binadamu ameumbiwa mitihani mingi, lakini moja kati ya mitihani hiyo ni kupewa uwezo wa kuhisi maumivu na hasira huku akiagizwa na Muumba wake kumsamehe anayemkosea na kumuombea mema adui anayepanga kumdhuru.

Huenda mtihani huu ndio uliosababisha mpigania uhuru wa India aliyefanikiwa, mmoja kati ya wanafalsafa ambao fikra zao zinaishi ingawa miili yao imelala, Mahatma Gandhi kusema, “watu dhaifu hawawezi kusamehe, kusamehe ni kielelezo cha tabia ya watu imara”.

Lakini falsafa hiyo ya Gandhi itaongezwa nguvu kwa mtu ambaye anasamehe sio kwa sababu hana namna ya kumuadhibu aliyemkosea, bali ana mamlaka yote na nguvu za kumuadhibu lakini ameyavumilia maumivu na kumsamehe aliyemuumiza.

Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameonesha uimara wa hali ya juu, akiwasamehe watu ambao wameonekana au kusikika hadharani wakimkashfu au kumtukana.

Licha ya kuwa na nguvu kubwa anayopewa na Katiba ya Nchi kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu, amejishusha akawakumbatia waliomtukana na kuwasamehe, ingawa amekiri kweli ‘inauma’.

Septemba 4, 2019, Rais Magufuli alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa pamoja wa wahandisi na wasanifu majenzi jijini Dar es Salaam, aliweka wazi kuwa amewasamehe Januari Makamba na William Ngeleja ambao walimtukana na akajiridhisha kwa asilimia zaidi ya 100 kuwa walitenda kosa hilo. Kumbuka mmoja alikuwa Waziri katika awamu yake na mwingine amewahi kuwa waziri katika Serikali zilizopita.

Kama hiyo haitoshi, jana Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye naye alipokea msamaha wa Rais Magufuli kwa kosa hilo hilo, kumtukana. Alimualika Ikulu, akamsikiliza, akamsamehe hadharani na zaidi akampa ushauri wa namna ya kupiga hatua kwenye maisha yake ya kisiasa. Akamtia moyo na kumuondoa wasiwasi! Hii ni ishara kuwa Rais Magufuli amefanikiwa kuushinda mtihani ule wa binadamu, ameonesha uimara na kuishi maandiko ya Mungu anayoyasoma, ingawa anakiri inauma.

“Inauma, kusamehe kunaumiza lakini ninasema kwa dhati kabisa kwamba nimemsamehe,” alisema Rais Magufuli alipokuwa akitangaza msamaha wake.

Katika Biblia Takatifu, neno ‘msamaha’ kwa lugha ya Kigiriki limeandikwa zaidi ya mara 146, na kwenye Quran Takatifu msamaha umetajwa zaidi ya mara 100 na rehema takriban mara 200. Hii inaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anasisitiza kusameheana. Ni maneno matatu makuu yanaweza kuiokoa dunia nzima, ‘msamha, upendo na rehema’.

“Unisamehe makosa yangu, kama ninavyowasamehe walionikosea.” Huu ndio mstari wa Biblia Takatifu, unaopatikana kwenye sala maarufu ya ‘Baba Yetu’ aliyoifundisha Yesu Kristo kwa wanafunzi wake, mstari ambao Rais Magufuli alieleza kuwa aliutafakari alipokuwa anausema anaposali na akaamua kuwasamehe Makamba na Ngeleja.

Je, kukasirika ni dhambi? La hasha, kukasirika sio dhambi kwani hata Mwenyezi Mungu hukasirika. Watu humuudhi Mungu, na watu huudhi watu, lakini Mungu aliyesema hata kama dhambi zako ni nyekundu kama bendera zitakuwa nyeupe kama dheruji atakapokusamehe anatutaka tuishi hivyo katikati ya maudhi na hasira.

Lakini matunda ya hasira yanaweza kuwa dhambi. Biblia inasema, “kuweni na hasira lakini msitende dhambi, jua silichwe na uchungu wenu bado haujatoka (Waefeso 4:26).” Katika Quran Takatifu, inaeleza jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anampenda mtu anayeweza kudhibiti hasira zake na kuwasamehe wenzake (Quran: Surah Al-e-Imran, Ayat 133-134).

Ni dhahiri Rais Magufuli alikasirika sana kusikia sauti za walivyokuwa wakimsema kwa lugha za ukakasi, lakini ameamua ‘jua lisichwe akiwa hajatoa uchungu wa maumivu’.

Ukiacha mbali kusamehe saba mara sabini kama alivyoeleza Bwana Yesu Kristo, Mwenyezi Mungu anatuagiza kusamehe na kusahau (inawezekana isiwe kufuta kumbukumbu lakini ni kutozifanya ziwe na madhara tena kwenye mawazo yetu). Rais Magufuli ameonesha hilo, amewasamehe Nape, Makamba na Ngeleja, amesahau na amemuelekeza aliyekuwa amemkosea njia bora zaidi ya kufanikiwa. Ameonesha kuwa hajabaki na chembe ya kinyongo, tena amemualika Ikulu kwa heshima kama mgeni wake wa heshima na sio mtu anayetaka kumpigia goti.

Mwanafalsafa mmoja alisema, “dunia ingekuwa sehemu salama zaidi ya kuishi kama watu wangekuwa wanasameheana na kupendana, na huenda watu wasingeyaona machungu ya kuishi duniani.”

Hata hivyo, Nape, Makamba na Ngeleja ambao walikosea wametufundisha somo kubwa la wazi. Wanapaswa kupongezwa pia na kuwa darasa huru kwa kila mmoja wetu.

Kwanza, kukosea tumeumbiwa binadamu. Hata Petro ambaye alipewa hadhi na Yesu kuwa ndiye ‘Jiwe’ ambalo juu yake atajenga kanisa, alimkosea Yesu lakini alipojuta na kutubu alisamehewa.

Tofauti na Petro, Yuda aliyemsaliti Yesu yeye hakuwa na muda wa wa kuomba msamaha, alienda zake akajimaliza mwenyewe, akafa na dhambi ya usaliti iliyomtafuna. Alisahau hatua ndogo baada ya kujuta, ‘kuomba msamaha’.

Marehemu Bluce Lee, Mfalme wa Karate, aliwahi kusema, “Makosa husamehewa daima, kama mkosaji atakuwa na ujasiri wa kuyakiri.” Makamba, Ngeleja na Nape walikuwa na ujasiri wa kuyakiri makosa yao na kuomba msamaha kwa dhati.

Nape amekuwa funzo zuri, ni kama Mungu amemtumia pia kutukumbusha binadamu sio tu kuomba msamaha, kuitafuta kwa dhati nafasi adhimu ya kuomba msamaha kwa tuliowakosea.

“Nape amekuwa akiomba msamaha, akiandika messages (jumbe) hata usiku wa manane, alikuwa anaomba anione… anione. Hata wasaidizi wangu wamekuwa wakiliona hili,” amesema Rais Magufuli.

“Amehangaika sana, ameenda hadi kwa Mzee Mangula [Philip Mangula], amefika mpaka kwa Mama Nyerere, amehangaika kweli lakini baadaye… ni katika hiyohiyo kwamba sisi tumeumbwa katika kusamehe. Na leo umemuona asubuhi amekuja hapa, nikaona siwezi kumzuia kuniona, kikubwa anachozungumza ni ‘naomba Baba unisamehe’,” ameongeza Rais Magufuli.

Wengine wasio na busara wameeleza utetezi wa kufunika makosa kuwa eti makosa yale yalifanywa kwenye faragha hivyo aliyeyafichua ndiye mkosaji!! Inashangaza!

Wanasahau kuwa hata Mungu wetu anajua kuna faragha, na Mungu pia yuko sirini. Lakini kuwa sirini hakumpi mtu yeyote ruhusa ya kufanya makosa. Kosa ni kosa haijalishi umelifanya kwa mazingira yapi, muhimu ni kukiri, kujuta na kuomba msamaha kama walivyofanya. Mwenyezi Mungu anatukataza kusengenya. Na kusengenya ni kumsema mtu kwa mabaya akiwa hayupo.

Kufanya kosa hakukuondolei hadhi yako endapo utakiri, kujuta na kuomba msamaha bali litabaki kuwa fundisho kwa wengine. Mfano, katika Biblia, Mungu alimfanya Mfalme Daudi kuandika makosa yake mwenyewe na hadi leo tunayasoma. Aliyafanya, alikiri, akajuta, akatubu na akasamehewa na akabaki kuwa ni mteule wa Mungu.

Kwa haya yaliyotokea ni dhahiri Rais Magufuli ameyaishi maandiko matakatifu na ameongoza kwa mfano. Tuendelee kumuombea. Tupo wengine huku mtaani, mbavu mbili tu na hata uongozi wa darasa hatujawahi kupata lakini tunavyopania kulipa visasi ni kama tuna mkataba na shetani. Tupo baadhi yetu ambao masikio yetu yakisikia tumetukanwa tunaweza ‘kuuza ng’ombe kwa kesi ya mbuzi’.

Tujifunze kwa rais wetu, vitabu vyote vitakatifu vinaelekeza kusamehe na kuepuka visasi. Pia, tujifunze kuepuka kuwakosea wenzetu na inapobidi umekosa kibinadamu omba msamaha, msamaha huokoa dunia. Ngoa nyingi zisingevunjika kama watu wangeombana msamaha wa dhati, vita nyingi duniani zisingetokea kama aliyekosea angeomba msamaha.

Mwenyezi Mungu aliisamehe dunia mara kadhaa baada ya watu kuomba msamaha; aliiteketeza Sodoma na Gomora kwa moto kwa sababu tu hakupatikana hata mtu mmoja mbali na Lutu aliyekuwa mwema ambaye aliomba msamaha. Maombi yetu kwa Rais Magufuli yanamfikia Mwenyezi Mungu, tunaona kwa vitendo kazi kubwa anayofanya na anavyoishi kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu.

 

Darasa la 7 kuanza mtihani wa Taifa leo
Video: Nape alivyoteseka kumuomba radhi JPM, Faru 9 waletwa kutoka 'Sauzi'