Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amezungumza kuhusu yeye pamoja na viongozi wenzake wa Chadema kutopata mwaliko kama ambavyo viongozi kutoka vyama vingine vya upinzani walivyoalikwa Ikulu na kufanya mazungumzo na Rais John Pombe Mgufuli.

Mbowe amesema kuwa chama chake licha ya kubeba ajenda ya maridhiano ya kitaifa hakikupata mwaliko wa Ikulu, na ameongezea kuwa hafahamu ajenda walizoitiwa viongozi wengine wa vyama vya upinzani.

“Sisi (CHADEMA) hatujapokea mwaliko wowote wa simu au wa maandishi na hatujui wenzetu wamealikwa kwa utaratibu gani na ajenda ilikuwa ni ipi, labda wao ndiyo waeleze. Sisi tulishaongea hadharani na tulishaandika barua ya kutaka maridhiano ingawa mpaka sasa hatujajibiwa,” amesema.

Ikumbukwe kuwa Jumanne ya Machi 3, 2020 Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, aliitwa Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo na Rais John Magufuli.

Mbali na Maalim Seif, viongozi wengine wa vyama vya upinzani waliokwenda Ikulu na kuteta na rais siku hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.

Ambapo baada ya viongozi hao kutoka Ikulu, kuliibuka mjadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kutoonekana Ikulu siku hiyo kwa uongozi wa chama kikubwa cha upinzani nchini, Chadema.

Bukombe: Familia zapoteza Ng'ombe kwa radi
TCRA yatangaza kushindanisha tuzo 17 sekta ya mawasiliano