Wakati ambapo wanatanzania wengi wanaonekana kutoelewa kinachoendelea ndani ya Ukawa baada ya subira ya muda mrefu ya kusikia utambulisho wa mgombea wa kiti cha urais kupitia umoja huo, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amewatoa wasiwasi.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara wa Chadema uliofanyika jana jijini Mwanza, Mbowe alisema Ukawa bado wako pamoja na watamtangaza mgombea wao muda utakapofika na kwamba watanzania watafurahi.

“Kwa sababu watanzania wanataka mabadiliko na wanaonesha kwa vitendo kwenye zoezi la uandikishaji wa wapiga kura. Watanzania wengi wamejiandikisha haijawahi kutokea, na wengi waliojiandikisha ni vijana,”alisema Mbowe. “CCM imeshamtangaza wa kwao. [Ukawa] tutamtangaza wa kwetu kimkakati na watanzania wote mtafurahi, aliongeza.

Katika mkutano huo uliovuta umati mkubwa wa watu, Chadema waliwatambulisha rasmi wabunge wawili kutoka CCM waliohamia katika chama hicho, Ester Bulaya (Mbunge viti maalum) na James Lembeli (Kahama).

Akiongea katika mkutano huo, Lembeli alisema kujiunga na Chadema ni majibu ya sala zake alizofanya na familia yake siku chache zilizopita.

“Tarehe 16 nilisali sana na mama yangu, na familia yangu na ndugu zangu kule kijini nilipozaliwa, nikimuomba mwenyezi Mungu anitoe kwenye nchi yenye laana anipeleke kwenye nchi yenye neema,” alisema Lembeli.

Ester Bulaya anatarajia kugombea ubunge kwa tiketi ya Chadema katika jimbo la Bunda linalokaliwa na Stephen Wasira. Lembeli alitangaza kugombea ubunge wa Kahama kupitia chama chake hicho kipya.

Ester Bulaya Ameikwepa Ngumi Ya ‘Tyson’ CCM
Man City Wajitia Kitanzi Kwa Kevin De Bruyne