Baada ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kutoka suluhu na Nigeria ‘Super Eagles’, straika mahiri wa Simba, Mussa Hassan Mgosi, ameibuka na kusema kuwa licha ya mabadiliko makubwa yaliyoonekana kwenye mchezo huo, matokeo hayo hayajakata kiu ya Watanzania.

Mgosi amesema hayo kutokana na Watanzania wengi kuwa na kilio cha muda mrefu kinachoilenga timu hiyo, ambapo wengi wangependa kuona timu hiyo inakuwa katika ramani ya ushindani kama zilivyo timu kubwa za barani Afrika.

Ikumbukwe kuwa Stars na Super Eagles, zilivaana juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, ukiwa ni mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki Afcon 2017 nchini Gabon.

Mgosi alisema kuwa kwanza kabisa anampongeza kocha mkuu wa kikosi hicho, Charles Boniface Mkwasa, ambaye ameonyesha kuwa anaweza kuifikisha mbali timu hiyo kutokana na utofauti wa timu ambao unaonekana sasa, lakini akasema ni lazima wachezaji wajiulize ni nini Watanzania wanahitaji, badala ya kufurahia kutoka suluhu.

“Kama utakuwa muungwana hautapingana na mimi kwa hii kauli ya kumsifu kocha wetu Mkwasa kwa mabadiliko aliyoyafanya kwenye kikosi cha Stars, lakini ni wakati wa wachezaji sasa kujiuliza ni nini hasa Watanzania wanahitaji kutoka kwao na siyo kutoka sare kwani hapo bado tuna kibarua kigumu kwa kuwa wao watajipanga zaidi katika mchezo wa marudiano na hapo tutakuwa ugenini, hivyo kujituma zaidi kunahitajika.

“Kiuhalisia mpira huwa haubadilishwi kwa siku moja tu, saa wala dakika, bali ni mchakato ambao unahitaji uvumilivu lakini Stars inatakiwa kuwa na uchu wa ushindi, hasa kwa kujituma kama wanavyofanya wengine,” alisema Mgosi.

Pogba: Nilikataa Kuihama Juventus
De Gea Ajitokeza Mtandaoni Baada Ya Juma Moja