Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Segerea kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro amesema kuwa rais John Magufuli amemshtua baada ya kutaja baraza lake la mawaziri.

Akiongea katika mahojiano maalum na Azam TV, Mtatiro alieleza kuwa kitendo cha rais Magufuli kutowataja mawaziri wanne katika baraza lake kwa kutoa sababu kuwa bado hajawapata kumemshtua kwa kuwa anaamini kuwa watanzania wenye uwezo wa kushika wizara hizo wapo wengi.

“Hakuna malaika, lakini watanzania wanaoweza kuteuliwa kuwa mawaziri wa wizara hizo wapo wengi tu,” alisema na kuongeza kuwa anaamini rais alikuwa na muda mrefu wa kulitafakari baraza lake tangu alipokuwa akifanya kampeni kwa muda wa miezi miwili pamoja na mwezi mmoja aliokuwa madarakani.

“Nimeshtuka kuona rais hajamtaja waziri wa fedha lakini amewataja mawaziri wengine. Yaani unateuwa watu wanaokuja kutumia fedha unamuacha mtu ambaye anatakiwa kukusanya fedha na kudhibiti matumizi yake,” Mtatiro aliongeza.

Mtatiro alishauri kutangazwa mapema kwa mawaziri hao waliobaki ili kazi ya kukamilisha serikali yake ianze mapema.

Ushauri huo wa Mtatiro unafanana na wito alioutoa gavana wa Kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei aliyemtaka rais Magufuli kukamilisha baraza lake mapema.

“Rais ameanza vizuri sasa na hao mawaziri lazima wamsadie kufanya kazi ya kupambana na wala rushwa na mafisadi,” alisema Mtei alipofanya mahojiano na gazeti la Mwananchi.

Home Shoppinga Center Yajitokeza Kujibu Tuhuma Za Kukwepa Kodi, wizi
Profesa Lipumba, Lissu wapinga uteuzi wa Muhongo na Mwakyembe