Fatma Karume, ambaye ni mtoto wa rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume amezungumzia mkwamo wa kisiasa visiwani humo uliotokana na tangazo la mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi huku akimshauri Dk. Ali Mohamed Shein kuachia madaraka.

Fatma Karume

Fatma Karume

Mwanasheria huyo wa kujitegemea ameeleza kuwa uamuzi wa kuondoka madarakani ni kuheshimu maamuzi ya wananchi wa Zanzibar walioufanya katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.

“Dk Shein ni lazima aondoke kwa sababu kuendelea kukaa madarakani ni kuwanyang’anya wazanzibari haki yao ya msingi,” Fatma alimweleza mwandishi wa gazeti la Mwananchi.

Aliongeza kuwa tangazo la Mwenyekiti wa ZEC kufuta uchaguzi sio halali kisheria kwani ni uamuzi binafsi usiotokana na kikao chochote cha Tume hiyo kinachotakiwa kuwajumuisha wajumbe wanne ili kupata baraka ya tamko la Tume. Alisema kuwa CCM wanakosea kusema kuwa Jecha ni Tume na Tume ni Jecha kwa kuwa sheria inaeleza bayana kuwa uamuzi wa Tume utafanywa kupitia kikao chenye akidi ambayo ni wajumbe wanne.

Akizungumzia dosari zilizojitokeza, Fatma Karume alieleza kuwa kama kulikuwa na ulazima wa kurudia uchaguzi, uchaguzi ungerudiwa Pemba kwenye majimbo ambayo dosari hizo zilijotokeza kama ilivyokuwa mwaka 2000.

Alisema kuwa mwaka 2000, chini ya uongozi wa aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamini Mkapa, kulitokea dosari kwenye baadhi ya majimbo Unguja na CUF walipotaka uchaguzi urudiwe wote walikataliwa na ukarudiwa katika majimbo yenye dosari pekee.

“Mkapa alisema wazi kwenye kipindi cha BBC cha Hard Talk akihojiwa na mtangazaji Tim Sebastian kuwa uchaguzi hauwezi kufutwa ila utarudiwa tu katika baadhi ya majimbo. Kwanini leo mambo yamebadilika na CCM wanataka uchaguzi mpya? Alihoji.

Mwanasheria huyo pia alieleza kuwa kuna tatizo katika kupitisha fedha za bajeti ya marudio ya uchaguzi kwakuwa bajeti hiyo ilipaswa kupitishwa na Baraza la Wawakilishi ambalo hivi sasa halipo kwa kuwa rais Shein alilivunja mwaka jana. Hivyo, endapo uchaguzi utarudiwa, fedha za bajeti ya uchaguzi hazitakuwa zimepitishwa na Baraza la Wawakilishi kama katiba inavyoelekeza.

“CCM imeshindwa Zanzibar kwa sababu imeshindwa kuwashawishi watu wake na badala yake inawakemea, ikawanyima haki zao. Kisaikolojia wapiga kura wanataka haki zao na wasibaguliwe lakini ukiwapelekea jeshi na vifaru, unazidi kuwapoteza,” Fatma Karume anakaririwa.

 

Siku ya Magufuli Kupewa Rungu la CCM Yabainika, Wajumbe Wagawanyika
Chozi la Sitti Mtemvu Laweka wazi Umri wake