Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania Mwinyi Zahera, amesema japokuwa wapo katika nafasi ya mwisho kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini bado anaamini kikosi chake hakitashuka Daraja msimu huu 2022/23.

Polisi Tanzania ilipoteza mchezo uliopita dhidi ya Dodoma Jiji FC iliyokua nyumbani Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Jumapili 9Machi 12) kwa kukubali kichapo cha 2-1.

Matokeo hayo yameifanya Polisi Tanzania kuendelea kushika nafasi ya 16 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 19, walizokusanya ndani ya michezo 25 waliyocheza hadi sasa.

Kocha Zahera amesema pamoja na kuwa katika mazingira mabaya ya kushuka Daraja, bado anaamini kikosi chake kina nafasi kubwa ya kupambana katika michezo iliyobaki na kujiondoa huko kilipo kwa sasa.

Amesema kimahesabu bado wana alama za kutosha ambazo zitawaondoka kwenye nafasi ya mwisho, endapo watashinda michezo iliyosalia msimu huu, na kazi anayoanza kuifanya hvi sasa ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake ili kushinda na kupata alama tatu za kila mchezo.

“Tupo kwenye nafasi ya mwisho, kwa inavyoonekana kuwa timu itashuka daraja moja kwa moja, lakini mimi kama Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania naamini bado tuna nafasi kubwa ya kubaki Ligi Kuu.”

“Tumebaki na michezo mitano, tukifanikiwa kushinda zote tutakusanya alama 15 ambazo jumla tutakuwa na alama 34 ambazo zitatuondoa moja kwa moja kwenye nafasi hatarishi.”

“Tunaendelea kujiimarisha zaidi ili kuhakikisha hatupotezi alama hata moja kuanzia sasa kwenye michezo hii tuliyobaki nayo kuhitimisha mashindano haya ya ligi.”

Michezo mitano ambayo Polisi Tanzania imebakiwa nayo, itacheza dhidi ya Singida Big Stars (ugenini), Ihefu (nyumbani), Mtibwa Sugar (nyumbani), Simba (ugenini) na Azam (ugenini).

Brahim Diaz ampagawisha meneja AC Milan
Christopher Galtier ang'ang'ana PSG