Hivi karibuni Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilimkamata mfanyabiashara aliyekuwa maarufu zaidi mitandaoni kupitia jumbe za masuala mbalimbali ya kisiasa aliyokuwa akiyaandika. Alikamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kutuma mtandaoni taarifa za upotoshaji.

Juzi, Yericco alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cypirian Mkeha na kusomewa mashtaka na mawakili wa serikali, Simon Wankyo na Paul Kadushi.

Mawakili hao wa serikali walieleza kuwa mshitakiwa alitenda kosa kwa kuchapisha kwenye mtandao wa facebook taarifa za upotoshaji kinyume cha sheria, huku wakizitaja jumbe mbalimbali zilizowahi kuandikwa na mshitakiwa huyo.

Kati ya jumbe zilizowasilishwa na wanasheria hao wa serikali ulisomeka kuwa “Piga Kura leo huku ukikumbuka kifo cha Mwangosi, mateso ya Ulimboka na Kibanda, mateso ya kijana wetu wa JKT, ukikumbuka hayo fanya maamuzi sahihi bila ushabiki.”

Ujumbe mwingine uliodaiwa kuwa aliuandika Oktoba 24 ulisomeka, “Umma umekosa amana na furaha, fursa pekee waliyoipata Watanzania ni kupiga kura kesho kukataa CCM na mambo yake yote. Watanzania wanamjua Rais wao wanayekwenda kumchagua kesho.”

“Mipango ya hujuma ya JK toka Ngurudoto Arusha na wakuu wote wa mikoa na wilaya Tanzania nzima, pia wakuu wa vyombo vya dola na wanadhimu mbalimbali. Wakuu wa Mikoa wanaelezwa kuwa NEC kwa kushirikiana na CCM tayari wameshatengeneza kura bandia kwa kutumia mfumo wa kalamu za China, pia wanaamuriwa kuhakikisha wanahujumu kampeni za Ukawa kwa kutumia vyombo vya dola.”

Hizo ni baadhi ya jumbe zilizotajwa kwenye mashtaka matano yanayomkabili Yericco Nyerere huku ikidaiwa mahakamani hapo kuwa alifanya makosa hayo kwa lengo la kuupotosha umma huku akifahamu kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Yericko alikana mashtaka yote na kuachiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti. Kesi yake imepangwa kusikilizwa kwa mara ya pili Decemba 1 mwaka huu huku upande wa serikali ukieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Tukio hilo limewashtua wengi ambao walihusika katika kusambaza taarifa mbalimbali walizokutana nazo kwenye mitandao zisizokuwa na uhakika huku nyingi zikiwa zenye mlengo wa kiushabiki zinazochafua upande fulani.

“Kama polisi wakiamua kufuatilia vizuri na kupekuwa mafaili ya facebook na instagram bila kupendelea upande mmoja wakati wa kampeni hadi uchaguzi mkuu, kwa mtindo huo wengi watapandishwa kizimbani kujitetea,” mtumiaji mmoja wa kijamii aliyejitambulisha kwa jina la Wambura aliiambia Dar24.

Sheria ya makosa ya kimtandao inakataza kuandika au kusambaza (kushare) habari za uongo au zenye mlengo wa upotoshaji, picha za utupu na zisizozingatia maadili, picha zinazowadhalilisha watoto na akina mama na mengine yanayofanana na hayo.

 

Beyonce, Tailor Swift wagombea ‘Umaarufu’ kwenye mitandao wa Kijamii
T.B Joshua Amebeba Ujumbe Muhimu Kwa Magufuli na Lowassa