Jeshi la Polisi limeanza kutekeleza agizo la Rais John Magufuli kwa kumpa kibali chenye masharti Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), kufanya mkutano wa hadhara kwa siku tofauti kuanzia mwezi huu ndani ya mipaka ya jimbo lake.

Kibali hicho cha polisi kimetolewa na Mkuu wa Polisi wilaya ya Iringa, OCD Y.Z Mjengi akijibu barua ya mbunge huyo aliyeomba kufanya mikutano katika jimbo lake ikiwa ni pamoja na mkutano wa hadhara wa Septemba Mosi, siku ambayo Chadema wametangaza kufanyika kwa Operesheni waliyoipa jina la ‘Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA’.

Kupitia barua yake kwa Msigwa, OCD Mjengi ameorodhesha masharti mengi anayopaswa kuyafuata Mbunge huyo wakati akifanya mikutano yake, ikiwa ni pamoja na kutomualika mtu yoyote kutoka nje ya jimbo lake kuzungumza katika mikutano hiyo.

“Mikutano yote hiyo kibali kimetolewa kwako kama Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini. Sitarajii mtu mwingine kutoka nje ya Mkoa wa Iringa kuja kukusemea kuhusu maendeleo ya jimbo lako au kuja kupokea kero za wananchi wako na kuzijibia wakati hiyo ni kazi ya mwenye himaya ambaye ni wewe,” alisema OCD Mjengi.

Aidha, Mkuu huyo wa Polisi Wilaya ya Iringa alimtahadharisha Msigwa kuangalia maneno atakayozungumza katika mkutano huo ikiwa ni pamoja na kutomkashfu mtu wa chama kingine pamoja na viongozi wa Serikali.

“Kashfa, Kejeli, matusi na maneno ya uchochezi kwa viongozi wa Serikali vitahesabiwa ni uvunjifu wa amani na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yako, na itapelekea kuzuiwa kufanyika kwa mikutano yako inayoendelea,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Hivi karibuni, Rais Magufuli aliwaelekeza wabunge waliochaguliwa na wananchi kupewa kibali cha kufanya mikutano ndani ya majimbo yao bila kuvuka mipaka ya jimbo hilo, kwa lengo la kuzungumza na wananchi kuhusu masuala ya maendeleo na sio vinginevyo.

Tundu Lissu awaka, avutana na agizo la Rais
Swansea City Wapingana Na Ashley Williams