Jeshi la Polisi jijini Mwanza, linawashikilia watu watatu kutokana na tukio la uvamizi wa msikiti wa Masjidi Rahman lililoko Nyamagana jijini humo lililosababisha mauaji ya waumini watatu na kuwajeruhi wengine.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi aliwaambia waandishi wa habari kuwa takribani watu 15 walivamia msikiti huo juzi wakiwa na silaha za jadi ikiwa ni pamoja na mapanga na shoka huku wakiwa wameficha sura zao wakijinadi kuwa wao ni magaidi.

Alisema kabla ya kutekeleza tukio hilo, watu hao walihoji kwanini waumini hao wanaendelea kusali wakati wenzao wamekamatwa na polisi.  Kamanda Msangi alisema baada ya swali hilo, walianza kuwakata waumini hao na kusababisha wakimbie hovyo na kupiga kelele.

Aliwataja waliouawa kuwa ni Imam wa Msikiti huo, Feruz Elias (27), Mbwana Rajab (40) na Khamis Mponda (28).

Mhanga wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina la Abed Makabwa, alisema kuwa watu hao walivamia msikiti huo na kuzima taa na kujitambulisha kuwa wao ni magaidi wakiwa wamejifunika sura zao, huku wakidai kuwa waumini hao wamewasaliti kwa kuendelea kusali wakati wenzao wamekamatwa na Polisi.

Alisema waliwataka wajitenge na watoto, na hapo ndipo walipopata mwanya wa kujichanganya na baadhi yao kufanikiwa kuwatoroka.

Maalim Seif atakiwa kukamatwa kwa kauli yake kuhusu Rais Shein
Lowassa atua tena Bungeni, awekwa kwenye mzani na Profesa Muhongo