Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amefanya tendo jema baada ya kusaidia kumuokoa mwanaume mmoja aliyetaka kujiua kwa kujirusha kutoka katika daraja liliko juu sana kutokana na kusumbuliwa na msongo wa mawazo.

Daraja hilo kubwa linaitwa Bosphorus, liko mjini Istanbul na linaunganisha bara la Ulaya na Asia.

Taarifa zilizoripotiwa na Associated Press, msafara wa rais Erdogan ulikuwa unapita katika eneo hilo na kubaini kuwepo kwa mtu huyo aliyekuwa anataka kujirusha kutoka juu ya daraja huku polisi wakijaribu kumsihi asifanye hivyo bila mafanikio kwa zaidi ya muda wa saa mbili.

Imeelezwa kuwa Rais Erdogan aliwataka wasaidizi wake kuongea na mtu huyo na kumsihi amfuate kwenye gari lake ili azungumze naye kwa kuwa alikuwa na mpango wa kumsaidia.

Rais Erdogan akizungumza naye akiwa ndani ya gari lake

Rais Erdogan akizungumza naye akiwa ndani ya gari lake

Baada ya kumsihi kwa muda, mtu huyo alikubali na kusaidiwa na maafisa wa polisi na wasaidizi wa rais kuelekea kwenye gari hilo na kuzungumza naye. Mwanaume huyo alimueleza Rais kuwa amekuwa akikabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo unaotokana na matatizo ya kifamilia hivyo alikata tamaa ya kuendelea kuishi.

Afisa mmoja wa Rais aliiambia Associated Press kuwa rais aliahidi kumsaidia mwanaume huyo ambaye baada ya kuongea naye alionekana kukubali kuwa mtulivu na kuendelea na maisha.

Utafiti: Mimba Nyingi Zaidi Hutungwa wakati wa Christmas
Kasi ya Magufuli Kumpitia Sumaye na Boss wa S.H Amon