Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema kuwa hana haraka ya kustaafu, na wala hana mpango wa kumwandaa mtu yeyote kurithi nafasi yake na badala yake anazingatia kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Uganda na bara la Afrika kwa ujumla.

Katika mawasiliano ya moja kwa moja na wafuasi wake kwenye mtandao wa kijamii wa facebook, Museveni amesema kuwa viongozi walio madarakani katika bara la Afrika, hawajaonyesha nia ya dhati kusuluhisha matatizo yanayolikumba bara hilo, na hivyo hawezi kuwa mwenye amani endapo atastaafu hii leo.

Rais Museveni ameyasema hayo wakati akiwa safarini kutoka Uganda hadi Yokohama nchini Japan, ambapo alitumia muda huo kuwasiliana na wafuasi wake kwenye mtandao wake wa kijamii, anaowaita kuwa wajukuu zake.

Aidha, wajukuu walimuuliza Museveni maswali mengi kuhusu hali ya Uganda, yanayowakera na yanayowafurahisha, wakiangazia masuala ya demokrasia, uchumi, na hali yao ya maisha.

Hata hivyo, Wafuasi wa rais Museveni kwenye mtandao wa kijamii wa facebook, wanamtaka astaafu na awe mshauri, wakipendekeza kwamba mbunge, Robert Kyagulanyi maarufu ‘Bobi Wine’ awe mrithi wake, wakiahidi kumtambua Museveni kama baba wa taifa na kumpa heshima za kitaifa.

Video: Saa 72 kuamua hatima ya ndege ya ATCL, Mshtakiwa aomba simu akatoe pesa
Dkt. Bashiru ampongeza Askari aliyegoma kutumia salamu ya CCM