Mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG) wanajipanga kumshawishi kwa mara ya tatu meneja wa Arsenal Arsene Wenger.

Wenger amewahi kuzipiga chini ofa mbili za klabu hiyo tajiri jijini Paris, kwa lengo la kuendelea kutimiza wajibu wake ndani ya klabu ya Arsenal ambayo alianza kuitumikia mwaka 1996.

Wenger mwenye umri wa miaka 67, anatarajia kumaliza mkataba wake na klabu ya Arsenal mwishoni mwa msimu huu, hali ambayo huenda ikawa rahisi kwa PSG kumuajiri kwa urahisi.

Dhamira ya kuajiriwa kwa mzee huyo, inapewa uzito na mmiliki wa klabu ya PSG Nasser Al-Khelaifi, ambaye hajaridhishwa na utendaji kazi wa meneja wa sasa Unai Emery aliyechukua jukumu la Laurent Blanc mwanzoni mwa msimu huu.

Tayari majina ya baadhi ya wakufunzi wa soka yamewasilishwa mezani kwa mmiliki huyo kama Roberto Mancini, Louis van Gaal na Clarence Seedorf, lakini Nasser Al-Khelaifi amesisitiza suala la kutaka kumuona Wenger akitua Parc des Princes.

Al-Khelaifi amejiandaa kumlipa Arsene Wenger mshahara wa Pauni milioni 10 kwa mwaka, huku akijiandaa kusikiliza lolote kutoka kwake kuhusu usajili wa wachezaji atakaowapendekeza.

Claude Le Roy Amuondoa Vincent Bossou Jangwani
Aliyekufa muda mfupi baada ya kubatizwa azikwa kiislam