Mkurugenzi mtendaji wa Mwanahalisi Publisher inayochapicha magazeti ya Mwanahalisi, Mseto na Mwanahalisi online, Said Kubenea amejiunga na mbio za kuwania ubunge wa jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chadema.

Akiongea na waandishi wa habari jana (Julai 21) baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chadema kugombea ubunge wa jimbo hilo, Kubenea aliwaambia wandishi wa habari kuwa amechukua uamuzi huo kwa kuwa anaamini Tanzania inahitaji mabadiliko.

“Nimeamua kugombea ubunge kwa sababu ninaamini taifa letu linahitaji mabadiliko. Na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema ‘wananchi wanahitaji mabadiliko, na wakiyakosa CCM kwenye chama chake, wataenda kuyatafuta kwenye chama kingine,” Kubenea aliwambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Jimbo la Ubungo hivi sasa linashikiliwa na mbunge wa Chadema, John Mnyika ambaye Kubenea amemshauri kuhamia Kibamba kwa kuwa tayari ameshafanya mengi katika jimbo la Ubungo.

Taarifa zisizo rasmi zinaeleza kuwa tayari John Mnyika alishafanya uamuzi wa kuliacha jimbo hilo na kugombea katika jimbo lingine ndani ya mkoa wa Dar es Salaam.

Kubenea ni mhariri nguli wa magazeti ya uchambuzi wa masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Alijipatia umaarufu zaidi kupitia makala zake na habari za uchunguzi zilizofichua maovu yanayofanywa na baadhi ya maafisa wa serikali na viongozi wa ngazi za juu.

Gazeti lake la Mwanahalisi hadi sasa linaendelea na adhabu ya kufungiwa kwa siku zisizojulikana hali iliyomsababisha kuanzisha ‘Mwanahalisi online’.

Arturo Vidal Kuitosa Juventus
Meek Mill Amponda Drake, Amkejeli Kwa Picha Aliyopozi Na Nicki Minaj