Serikali imesema itaendelea kufanya biashara na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia fursa zilizopo nchini ikiwemo uwekezaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Profesa Beno Ndulu alipokuwa akifungua mkutano wa Magavana na Manaibu Gavana kutoka nchi 14 za Mashariki na Kusini mwa Afrika unaosimamiwa na Taasisi ya Usimamizi wa Fedha na Uchumi kutoka (MEFMI).

“Tanzania imeanza miaka 2 hadi 3 kujiwekea akiba ya sarafu ya Yuan ya nchini China kutokana biashara mbalimbali ambapo hadi sasa nchi ina akiba ya asilimia 5 za fedha ya China Yuan” alisema Profesa Ndulu.

Hatua hiyo ya Tanzania inafuatia Sarafu ya China ijulikanayo kama Yuan kuingizwa kuwa miongoni mwa sarafu sita zinazotumika Duniani.

Mkutano huo unafuatia majumu ya Benki Kuu hizo za nchi wanachama kuwa na jukumu la kuwa walinzi wa akiba ya fedha za kigeni na wawezeshaji wa masuala ya biashara za kimataifa.

Maweneo ambayo Tanzania inayatumia kama njia moja wapo ya kujiongezea sarafu ya China ni pamoja na uwekezaji katika hati fungani inafaida zaidi ikilinganishwa na nchi za Ulaya na nchi nyingine duniani.

Profesa Ndulu alizitaja sarafu nyingine ambazo zinatumika duniani zinazotambuliwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ni pamoja na Dola ya Marekani, Euro inayotumiwa na nchi za Ulaya, Swiss Frank ya Uswiss, Paund ya Uingereza, Yen ya Japani pamoja na Yuan ambayo itaanza kutumika kimataifa kuanzia mwezi Septemba 2016.

Mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na China ni ya kihistoria yanayohusisha Serikali za nchi hizo mbili ambao ulijengwa kwa msingi imara wa Waasisi wa mataifa hayo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Muasisi wa Taifa la China Mwenyekiti Mao Tse Tung.

Mkutano wa huo wa MEFMI unatoa fursa ya kipekee kubadilishana mawazo kwa viongozi hao juu ya ushirikishwaji wa Yuan Kichina ndani ya kikapu cha hifadhi ya sarafu ya IMF / Benki ya Dunia katika nchi wanachama wa MEFMI.

Kufanyika kwa mkutano huo ni moja matukio ya kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yanayotarajiwa kutahudhuriwa na Wachumi waliobobea wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo magavana 20 kutoka nchi za Jumuiya ya  Afrika  Mashariki  (EAC)  na  wa  Jumuiya  ya  Maendeleo  ya  Nchi  za  Kusini  mwa  Afrika (SADC).

Shirko aja na mtindo mpya wa Muziki, aubatiza majina haya
Tanzania kupunguza vifo vya watototo wadogo vitokanavyo na Malaria.