Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa bado anasubiri majibu ya kuondolewa kwa kodi ya gharama za taulo za kike (Pedi) ili kuweza kuondokana na tatizo linalowakumba watoto wa kike wakati wa siku zao.

Ameyasema hayo hii leo Bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalum, Stella Ikupa aliyehoji kuhusu serikali kufanya maamuzi ya haraka kuhusiana na kodi zinazopelekea taulo za kike kuuzwa kwa bei ghali huku wanaoathirika wakiwa ni watoto wa kike wengi wasiokuwa na uwezo wa kugharamia.

“Nikiwa kama Waziri wa Afya lakini pia ni mama mwenye watoto wa kike  nikiri kwamba changamoto katika jambo hili ni kubwa sana. nakiri wapo wanafunzi wanaokosa masomo hata kwa siku tano kwa mwezi ili kujihifadhi kutokana na kutokuwa na taulo salama, lakini wapo wanaotumia mpaka majani.  Ombi la kuondoa kodi nimeshalipeleka kwa waziri wa fedha na hata sasa nilikuwa namtafuta humu ndani ili kumsihii aharakishe mchakato huu,”amesema Ummy Mwalimu

Aidha, Kwa upande wa Naibu Waziri wa Afya Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa maamuzi kuhusu kuondolewa kodi kwa taulo hizo yalishawasilishwa bungeni mara kadhaa lakini pia maamuzi kamili yamekuwa yakichelewa kutoka kutokana kuwa bidhaa hizo hazijawahi kuorodheshwa kama vifaa tiba.

Hata hivyo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewataka wabunge wanawake kusimamia kuondolewa kodi katika taulo hizo za usafi za kike ‘pedi’ kutokana na kutozwa kodi kwani zimekuwa zikiuzwa kwa gharama kubwa hali inayowafanya wanawake wengi kushindiwa kumudu kuzinunua

Aliyekuwa Mkurugenzi ATCL ahukumiwa miaka 6 jela
JPM amfutia Manji umiliki wa eneo Kigamboni