Mlezi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara, Waziri mkuu mstaafu wa awamu ya nne  Mizengo Pinda amewataka watanzania waendelee kukiamini chama hicho kwa kuwapigia kura madiwani,wabunge na rais ifikapo Oktoba 28,2020.

Pinda ameyasema hayo mjini  Babati  wakati akimnadi kwa wananchi  mgombea ubunge wa jimbo hilo Paulina Gekul,  katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Papaa. 

Waziri mkuu wa serikali ya awamu ya tatu , Fredrick Sumaye ambaye pia alishiriki katika uzinduzi huo amewataka wakazi wa Manyara kupuuza  maneno ya watu wanaowasema vibaya mgombea ubunge Paulina Gekul na mgombea urais John Magufuli .

Kwa upande wake, Gekul  amesema serikali imefanya mengi katika Jimbo la Babati na kata zake nane kwa kuleta maendeleo katika nyanja zote ikiwemo Elimu,Afya na Miundombinu.

Amesema kupitia Serikali ya  CCM, kata zote katika jimbo hilo zinapitika kwa kuwa barabara zote zimechongwa na TARURA na kwamba katika kipindi kijacho cha awamu ya pili,  wanatarajia kupokea mradi mwingine wa lami zaidi ya kilomita 35 ambazo zitaondoa vumbi katika mji huo.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020,  Pinda ni Mratibu  wa kamati za Kampeni  katika mikoa ya Manyara, Arusha,Kilimanjaro na Tanga.

Geita, Kahama kuunganishwa kwa lami
Tanzania kuanza kusafirisha nje mbegu asili za mboga