Mshambuliaji wa kutumainiwa katika klabu ya Nice ya nchini Ufaransa, Super Mario Balotelli kwa mara ya kwanza amezungumzia matamanio ya kuitwa tena katika kikosi cha timu ya taifa ya Italia.

Balotelli amesema anatamani kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa lake kwa sasa, kutokana na kiwango chake kuendelea kuimarika siku hadi siku, tangu alipohamia nchini Ufaransa.

Hata hivyo mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, amesema hana haraka ya wito huo, zaidi ya kutaka kuendelea kuuthibitishia umma wa mashabiki kuhusu uwezo wake wa kucheza soka na kufunga mabao.

“Ninasisitiza, ninasubiri kuitwa katika timu ya taifa, lakini sio kwa lazima, kutokana na kuamini kwamba wakati utakapowadia kocha ataniita,” Balotelli aliliambia gazeti la michezo ya nchini Italia (Gazzetta dello Sport).

“Kama hali ya kutoitwa kwenye kikosi cha Italia itaendelea, sitojali, kwa sababu najua huenda kiwango changu kitakua bado hakijakua kwa kiasi ambacho kitamridhisha kocha Giampiero Ventura,

“Nitaendelea kucheza kwa bidii ili nifikie kiwango ambacho kitamridhisha na kuniita kwa ajili ya kusaidiana na wengine watakaotajwa kikosi kwa kipindi kijacho.”

Video: 'Bodi ya mikopo haijajipanga' - Sauti Zetu
Slaven Bilic: Tunajivunia Kuwa Na Payet