Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) jana iliwahoji Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na Mbunge wa Nzega Mjini (Hussein Bashe) kutokana na tuhuma za rushwa zinawakabili baadhi ya wabunge.

Bashe

Hussein Bashe

Zitto na Bashe ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii walihojiwa na Takukuru kwa zaidi ya saa mbili, ikiwa ni siku chache baada ya kuwasilisha kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, barua za kujiuzulu katika Kamati hiyo wakitaka uchunguzi kufanyika.

Zitto alithibitisha kuhojiwa na Takukuru na kudai kuwa amefurahishwa na namna mahojiano yalivyofanyika.

“Nafurahi wito wetu wa uchunguzi umechukuliwa kwa uzito unaostahili na tutatoa ushirikiano wote kwa vyombo vya uchunguzi ili tumalize zoezi hili kwa haraka na kwa ufanisi,” Zitto alinukuliwa.

Naye Bashe, licha ya kuthibitisha kufanyiwa mahojiano na Takukuru, alieleza kuwa amebaini chombo hicho kilianza kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za rushwa kwa Wajumbe wa Kamati za Bunge kutoka kwa Mashirika mbalimbali ya Umma, hata kabla habari hizo hazijafahamika kwa umma kupitia vyombo vya habari.

Mbali na wabunge hao, Takukuru imewahoji pia wabunge wengine saba kutokana na tuhuma hizo ingawa majina yao hayakutajwa mara moja.

Hivi karibuni, Spika wa Bunge, Job Ndugai alizipangua Kamati za Bunge kimyakimya huku ikielezwa kuwa ni kutokana na tuhuma hizo za rushwa. Hata hivyo, Ndugai aliviambia vyombo vya habari kuwa amefanya mabadiliko hayo sio kutokana na kusukumwa na tuhuma hizo bali ni kawaida kama kocha anavyopangua timu yake.

Ndugai alisema kuwa Bunge sio chombo cha uchunguzi, hivyo vyombo husika vinapopata habari kama hizo ni jukumu lao kufanya uchunguzi.

Video Mpya: Vanessa Mdee - Niroge
Hendrik Johannes Cruijff Afariki Dunia