Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), imedhamiria kukusanya mapato makubwa ya kuipatia serikali na kuweza kujiimarisha, huku ikibainisha kuwa itahakikisha misingi, taratibu na kanuni za taasisi za umma zilizowekwa zinafuatwa na wafanyakazi wa taasisi hiyo ili kuweza kufikia lengo hilo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi mpya wa TPA, Erick Benedict Hamis wakati akizungumza na Dar24 kuhusu vile ambavyo amejipanga kwenda kufanya kazi katika taasisi hiyo, ambayo Mkurugenzi wake wa zamani amesimamishwa kazi na Rais Samia Suluhu kutokana na upotevu wa fedha zaidi ya Shilingi Bilioni tatu.

“Tuna muda mfupi sana wa kufanya mabadiliko chanya, hii ni taasisi ya umma na inaongozwa na kanuni, misingi na taratibu za umma, kwa hiyo tutaenda kuangalia ndani ndani ya taratibu hizo na misingi na kanuni, je zinafuatwa sawa?, miradi ya maendeleo, operesheni, je zinaenda inavyotakiwa?,” amesema Erick.

Erick ameeleza kuwa bandari ndiyo lango la uchumi wa nchi, na TPA ni taasisi kubwa yenye mapato makubwa hivyo hawana budi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuweza kutekeleza hilo ndani ya muda waliopewa na Rais Samia.

Awali akizungumza mara baada ya uapisho wa viongozi Aprili 6, 2021, Rais Samia alimuagiza Erick kuhakikisha ufanisi wa Bandari nchini unaimarika ndani ya kipindi cha miezi Sita.

“Erick ulikuwa Dar es Salaam kwa sababu moja au nyingine ukatupwa Mwanza, hukuvunjika Moyo ukafanyakazi Mwanza na Mwanza umefanyakazi nzuri sana, baada ya kuona ubadhirifu na yaliyopo hapa nikasema nikutoe Mwanza nikulete Dar es Salaam, imani yangu kazi uliyoifanya Mwanza Dar es Salaam utaifanya mara mbili,” alisema Rais Samia.

“Unajuana na watu wa Dar es Salaam nenda pale usiangalie mtu usoni najua ndani ya Bandari kuna makundi mawili kuna makundi hili na lile, unakwenda pale huna kundi nenda kafanyekazi simamia kwenye mstari muda wangu ni miezi sita Erick nitaangalia hali ya Bandari inavyokwenda alafu tutakuja akizungumzia mengine baadaye,” alisisitiza Rais Samia.

Simba SC yawasili Cairo, Misri
Hitimana Thiery afichua siri nzito Mtibwa Sugar