Hatimaye kitendawili cha tano bora kimetenguliwa na kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana hadi usiku wa manane mjini Dodoma.

Kwa majibu wa taarifa za kuaminika kutoka mjini humo, kikao hicho kimewapitisha Bernard Membe, January Makamba, John Magufuli, Asha Rose Migiro na Amina Salum Ali.

“Hayo majina, kwa taarifa nilizozipata dakika mbili baada ya mheshimiwa Nape Nnauye kuzungumza ndio ukweli,” Chanzo hicho cha kuaminika kiliiambia Clouds Fm mapema leo asubuhi.

Hata hivyo, chanzo hicho kimeeleza kuwa Nnape Nauye hakuyataja majina hayo lakini waliyapata majina kwa ufuatiliaji muda mfupi baada ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa kuzungumza na waandishi wa habari na kudai kuwa hawakubaliani na majina matano yaliyopitishwa na chama hicho.

Dr. Nchimbi ameeleza kuwa hawakubaliani na utaratibu uliotumika kuyapata majina hayo kwa kuwa majina yaliyopitiwa ni machache zaidi ya yale yaliyopaswa kuwasilishwa.

Habari hizo pia zimethibitishwa na akaunti ya Twitter ya CCM iliyoyataja majina hayo matano. Muda mfupi ujao, chama hicho kitafanya mkutano na waandishi wa habari katika eneo la St. Gasper ili kutoa taarifa rasmi.


Majina matatu kati ya majina hayo yanatarajiwa kuchaguliwa leo na NEC kabla ya kumtaja mmoja mapema kesho.
Imeelezwa kuwa hali ya usalama mjini humo imeimarishwa kupita kiasi na kwamba kila mtu aliyepo katika mji huo amepaswa kuwa makini sana.

Newcastle Utd Kuongeza Majembe
UKAWA Wachujana Kupata Jembe La Urais