Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amemteua Lowata Sanare kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, akichukua nafasi ya aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Stephen Kebwe.

Akitangaza uteuzi na utenguzi huo leo Septemba 20, 2019 Katibu mkuu kiongozi  Balozi Mhandisi John Kijazi, ameeleza kuwa Rais amefanya uteuzi na mabadiliko kadhaa.

Aidha Rais Magufuli amemteua Musa Masele ambaye alikuwa msaidizi wa Mkuu wa mkoa wa Geita, kuwa mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mkoani Morogoro.

Ikumbukwe kuwa Kebwe aliwahi kupewa maonyo juu ya utendaji wake na Rais Magufuli, Waziri  Mkuu pamoja na DK Bashiru .

Juzi katika ziara ya Waziri Mkuu mkoani Morogoro alimwambia achunge mkoa wake kwani hali ni mbaya kila kona ”Mkuu wa mkoa chunga mkoa wako hali ni mbaya, kila wilaya hali ni mbaya upotevu wa fedha ni mkubwa mno, mkoa wa Morogoro ni shida”.

Rais Magufuli alitoa onyo Julai 25 wakati aliposimama kwa muda eneo la Kisaki Mkoani Morogoro na kuzungumza na wananchi wakati akiwa njiani kwenda Mto Rufiji kuzindua mradi mkubwa wa uzalishaji umeme katika bonde la Stigler.

Magufuli alimtaharisha kuwa siku nyingine atakapo pita Morogoro na kukuta tatizo la wafugaji kupeleka mifugo kwenye mashamba ya wakulima linaendelea ataona viongozi hawatoshi.

Aidha Dk Kebwe jana alipozungumza na gazeti la Mwananchi kuelezea utendaji kazi wake na maoni yake juu ya matamko ya viongozi hao wa juu na hali tete ya wadhifa wake alisema kuwa hatua zimekuwa zikichukuliwa na kitendo cha Waziri Mkuu ni cha kupigilia msumari kile wanachokifanya..

Mbali na uteuzi huo, Rais amefanya mabadiliko ambapo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Charles Kabeho, amehamishiwa wilaya ya Chato na Mkuu wa Wilaya ya Chato Msafiri Mtemi amehamishiwa Wilaya ya Tarime.

[youtube https://www.youtube.com/watch?v=Q6hv1-Jzh9s]

Fatma Karume asimamishwa uwakili
Viongozi wanne Chadema mbaroni