Kocha wa Mwadui FC ya mkoani Shinyanga Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ amewageukia waamuzi wa mchezo wa African Sports vs Mwadui FC na kuwatuppia mzigo wa lawama mara baada ya timu yake kukalishwa kwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga kwenye mchezo wa ligi kuu uliochezwa juzi February 3.

Julio amesema mara nyingi amekuwa akiwasifia waamuzi bila kujali kama timu yake imefungwa wala imeshinda bali huangalia kama wamechezesha kwa haki na kwa kufuata sheria zote za mchezo wa soka.

“Kilasiku nimekuwa nikiwapongeza waamuzi iwe tumeshinda au tumefungwa. Nimefungwa na Azam lakini niliwasifia waamuzi, nimefungwa na Mbeya City nimewapongeza waamuzi nikafungwa tena na Mtibwa Sugar sikuacha kuwapongeza waamuzi. Pamoja na kufungwa kwetu lakini walikuwa wanachezesha vizuri”.

“Adongo alikataliwa juzi kwenye mechi ya Kagera na Mbeya City kwa kuonekana alifanya vibaya kwa kuionea Kagera, leo kwenye mechi yetu katoa maamuzi mabovu kwa kutufungisha goli la penati ambalo siyo, hata watu wa Tanga wenyewe walikuwa wakituhurumia kwa jinsi alivyokuwa anafanya hata tungecheza dakika 600 tusingeshinda”.

“Tatizo kubwa la waamuzi wetu ni kutojielewa leo wanafanya hivyo kwa kutaka kuinusuru African Sports na kiongozi mmoja mkubwa wa serikali sitaki kumtaja anawaambia waamuzi fanyeni kama tulivyokubaliana”.

Mechi ijayo Mwadui itakutana na Azam FC kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

 

Spurs Wamuwekea Uzio Josh Onomah
Kikosi Cha Mbeya City Kunolewa Na Phiri