Wabunge wa chama tawala cha Democrats nchini Marekani jana walisusia vikao vya Bunge kwa mtindo wa aina yake wakishinikiza kupigiwa kura na kupitishwa kwa sheria kali ya udhibiti wa umiliki silaha nchini humo.

Tukio hilo limetokea wakati bado kuna mjadala na ubishani mkubwa kuhusu sheria ya udhibiti silaha inayopendekezwa, hali iliyochochewa zaidi na tukio la mauaji ya watu 49 katika klabu ya usiku huko Orlando, Florida.

Mmoja kati ya wabunge hao, John Lewis alisikika akiwahimiza wabunge wenzake kuhakikisha hawakati tamaa hata kidogo hadi sheria kali ya udhibiti wa silaha ipitishwe.

Wanataka Bunge liendelee na vikao vyake kwa wiki nzima kujadili suala hilo na kulipitisha, hoja inayopingwa na wenzao wa chama cha Republican.

Wabunge hao wanaotoka chama alichopo Rais Barack Obama wanaunga mkono kile anachokipigania Rais huyo ambacho kimekumbwa na upinzani mkali hasa kwa baadhi ya vipengele vinavyominya zaidi umiliki wa silaha nchini humo.

Hata hivyo Spika wa Bunge hilo Paul Ryan, kutoka chama cha Republican ametupilia mbali hatua hiyo ya kukaa sakafuni kusema hiyo ni mbinu ya kujitangaza kisiasa

January mwaka huu, rais Obama alitokwa na machozi wakati akitoa hotuba yake kutetea muswada wa sheria ya kudhibiti umiliki silaha kutokana na matukio ya mauaji yanayotokana na watu kuwafyatulia risasi watu katika sehemu mbalimbali wanazokutana.

Iceland Yasonga Mbele Euro
Mmiliki Wa TP Mazembe Ahukumiwa Kifungo