Wapinzani wa Yanga katika michuano ya Kombe la Kagame, Gor Mahia FC wamesema watajitoa katika michuano hiyo iliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 18 baada ya kuibuka kwa utata katika suala la tiketi za ndege kusarisha timu yao kutoka Kenya.

Jana Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lilitoa taarifa ya kuthibitisha kwamba halitalipia tiketi za ndege kuisafirisha timu ya Gor Mahia likieleza kuwa haliko katika hali nzuri kuwawezesha mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kufika Dar es Salaam.

Katibu mkuu msaidizi wa Gor Mahia,Ronald Ngala, amekaririwa na mtandao wa Futaa.com leo akieleza kuwa tayari wameshatuma barua CECAFA kulitaarifu Baraza hilo la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati kuhusu kinachoendelea katika kutafuta namna ya kuisafirisha timu kuja Tanzania na kwamba baraza hilo limeahidi kumaliza tatizo hilo.

“Katika michuano iliyopita, tiketi za ndege kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame zilikuwa zinatolewa na CECAFA, lakini tumeambiwa kuwa katika mkutano mkuu uliopita wa vyama vya soka vya nchi wanachama wa baraza walikubaliana kila shirikisho litawajibika kulipia gharama za usafiri wa ndege wa timu zinazowakilisha nchi husika katika michuano na hii ndiyo sababu iliyotufanya tuiandikie barua FKF kuomba tiketi zetu,” amesema Ngala na kuongeza:

“Baada ya FKF kutuambia kwamba haiwezi kutulipia tiketi za ndege, truliandika barua kwenda CECAFA Jumatano (jana) kuwataarifu kinachoendelea na walituahidi kutupa mrejesho. Timu yetu iko kamili na tumejiandaa kufanya vyema katika mashindano haya.”

Gor imepangwa Kundi A pamoja na wenyeji Yanga, Khartoum ya Sudan, Telecom FC ya Ethiopia na KMKM ya Zanzibar. Michuano hiyo itaanza Jumamosi Julai 18 na kumalizika Jumapili Agosti 2. Gor Mahia itafungua michuano kwa kuivaa Yanga Julai 18.

Recho Ajibu Tuhuma Za Kutumia Dawa Za Kulevya
Okwi Akamilisha Alichokitilia Nia Denmark