Katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya wakulima (nane nane) Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kasim Majaliwa, amesema kuwa  amefurahi kuona wakulima, wafugaji na wafanyabiashara wa mazao, pembejeo na zana za kilimo wana ari kubwa ya kushiriki katika kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya kuifanya nchi kujitosheleza kwa chakula na kuendeleza uchumi wa viwanda.

Waziri Mkuu amesema wakulima wanatakiwa  kuzingatia matumizi ya kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya zana za kisasa, pembejeo na viuatilifu vilivyopendekezwa na wataalam ili kufanikisha mapinduzi ya kilimo kuelekea kilimo cha biashara.

“Naamini kuwa pamoja na lengo la kujitosheleza kwa chakula, wakulima, wafugaji na wavuvi wataongeza ari ya uzalishaji kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi katika kuvipatia viwanda vyetu malighafi na kuongeza thamani ya mazao,”- Majaliwa.

Aidha katika hatua nyingine Mh. Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuweka mikakati endelevu ya kuwawezesha wananchi kuvua katika maji ya kina kirefu cha bahari kwa kutumia meli kubwa na za kisasa ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali hiyo ambayo imekuwa ikichukuliwa na wavuvi wenye vyombo vya kisasa kutoka nje ya nchi.

Sanjari na hayo amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaweka mikakati na mipango ya kuifanya mito na maziwa mbalimbali nchini kuwa na uvuvi endelevu kwa kufuatilia kwa karibu shughuli za wavuvi na kuwaadhibu wote watakaovua kinyume na sheria.

Akizungumzia kuhusu suala la usindikaji nchini Waziri Majaliwa alisema wakati anatembelea mabanda mbalimbali alipata fursa ya kuona teknolojia zinazoweza kutumiwa na wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuongeza uzalishaji bora wenye tija.

Leo Agost 1 Waziri Mkuu amezungumza hayo yote wakati akifungua maadhimisho ya 23 ya sherehe za maonesho ya wakulima Kanda ya Mashariki katika Uwanja wa Mwalimu J.K Nyerere yanayofanyika katika mkoa wa Morogoro ambapo Kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ni ”kilimo, mifugo na uvuvi ni nguzo ya maendeleo Vijana shiriki Kikamilifu”

 

 

Uturuki yakamata Makomando waliotaka kumteka Rais
Wadau Wa Michezo Watakiwa Kushirikiana Na Serikali Kuinua Michezo