Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewataka Wakuu wa Shule mkoani humo kuongeza ubunifu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika shule zao.

Ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili kwa wakuu wa shule zote za Sekondari yaliyofanyika Mjini Bariadi, mkoani Simiyu alipowataka waalimu hao kuwa wabunifu.

Amesema kuwa wakuu wa shule wanatakiwa kuwa wabunifu hususani katika mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuwaandaa vizuri kitaaluma wanafunzi ikiwa ni pamoja na mazoezi na mitihani ya kujipima ya mara kwa mara, zitasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani ya ndani na kitaifa.

“Kiongozi lazima uwe mbunifu, Mkiwa wabunifu kwenye shule watoto watafanya vizuri,mnapaswa kubuni mbinu na mikakati mbalimbali kwenye majaribio ya darasani, mitihani ya kujipima na  kubuni namna ya kuwapa motisha walimu wenu wapende kazi na kujiona ni wanafamilia katika shule mlizopo” amesema Mtaka.

Aidha, amewataka wakuu hao wa shule kujiwekea utaratibu wa kupita mara kwa mara madarasani kukagua kwa lengo la kujiridhisha, ikiwa walimu wanatimiza wajibu wao wa kuwafundisha wanafunzi kama inavyotakiwa badala ya kusubiri kuletewa taarifa.

Mkuu huyo wa Mkoa pia amewaasa wakuu hao wa shule kuwa na uongozi shirikishi ambao unajali pande zote kwa maana ya walimu, wanafunzi na wazazi ili waweze kujua kero na masuala mbalimbali yasiyowaridhisha na waweze kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu kuyapatia suluhu.

Hata hivyo, amesisitiza wakuu wa shule kufanya vikao na wazazi kwa kuwa wazazi wanayo nafasi kubwa ya kuchangia wanafunzi kufanya vizuri, hivyo akawataka wavitumie vikao kupata maoni ya wazazi katika masuala mbalimbali ya kuboresha maendeleo ya wanafunzi kitaaluma.

 

Kagame aongoza kwa kura nyingi uchaguzi mkuu Rwanda
Magazeti ya Tanzania leo Agosti 5, 2017