Watu saba wamefariki kwenye ajali iliyotokea usiku wa kuamkia leo Juni 22, 2021 katik eneo la nanenane Oilcom karibu na stendi kuu ya mabasi mkoani Morogoro na kuhusisha magari matatu ambayo ni Toyota Coaster yenye usajili namba T189 PUK, Toyota Cresta T563 ASA na gari aina ya roli T658 BJZ kampuni ya Dangote.

Akizungumza na Dar24Media kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Morogoro Fortunatus Musilimu amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Coaster lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Mbeya baada ya kuovateki bila kuwa makini huku akiwa kwenye mwendokasi na kusababisha ajali hiyo kutokea na kusababisha vifo vya watu watano palepale na wawili walifariki wakipata matibabu na kufanya idadi kufia saba.

“Dereva aliovateki bila kuchukua tahadhari ya magari mengine na akiwa katika mwendo mkali alipoona mbele yake kuna Roli akarudi upande wa kushoto na ndipo akaligonga gari la pili cresta na ndipo gari la coaster likapoteza muelekeo kurudi tena upande wa kulia na kwenda kugongana na Lori na kusababisha ajali,” amesema Kamanda Musilimu.

Kamanda Musilimu amesema jumla ya majeruwi ni 24 wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa Morogoro na kati yao 17 wanaendelea vizuri na matibabu na Saba walipata majeraha makubwa pia wanaendelea na matibabu.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linafuatilia gari la coaster lililosababisha ajali kama linakibali cha Latra, kutokana na kuweka mashada ya maua kuonyesha wamebeba jeneza kwenda mazikoni lakini hakukuwa na jeneza kuonekana ikiwa ni mbinu ya kukwepa mapolisi wa doria usiku, pia inasemeka gari hilo lilikuwa limebeba wafanyabiashara waliokuwa wakielekea mbeya na kugeuza kesho yake yani leo Juni 22 kuja Dar es Salaam.

“Kwahiyo unaweza kuona kwamba gari hili lilitoka kiwiziwizi kwaiyo tunafuatilia kuona kwamba linakibali au la tutawasiliana na watu wa LATRA kuweza kuona kama gari hili lina kibali cha kutoka Dar kwenda Mbeya,” amesema Kamanda Musilimu.

Utambuzi wa miili ya marehemu na majeruhi umeanza leo Juni 22 katika Hospitali ya Rufaa Morogoro.

Kamanda Musilimu ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo na kuwaasa wananchi kutoa taarifa endapo wanaona dereva anakiuka sheria za barabarani.

Mabadiliko ya vitambulisho vya wajasiriamali
Jokate awashukuru Kisarawe, aahidi Temeke mpya