Wataalamu wa mazingira nchini, wametakiwa kutumia vyema fursa za mafunzo yanayotolewa na wadau wa maendeleo, ili kuibua ajenda na vipaumbele muhimu vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga ameyasema hayo wakati wa hotuba yake ya kufunga Warsha ya siku mbili ya wadau na Wataalamu wa Mazingira inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na Mazingira wa Dunia (GEF), na kusomwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Dkt. Andrew Komba.
Amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na GEF imeandaa warsha hiyo kwa ajili ya kuwakutanisha wataalamu na wadau wa mazingira ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya GEF mzunguko wa nane ambao unatarajia kutekelezwa katika kipindi cha miaka minne ijayo.
“Warsha hii ilikuwa na malengo makuu mawili ambayo ni kuanisha vipengele vya miradi ya GEF mzunguko wa nane na pia kupeana ujuzi na maarifa ya pamoja katika namna ya kukabiliana na athari za mazingira na mabadiliko ya tabia nchi” amesema Bi. Maganga.
Aidha, Bi. Maganga amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekuwa ikiendesha mafunzo na warsha mbalimbali ili kuhakikisha kuwa wataalamu na wadau wa mazingira wanaongeza ujuzi na maarifa katika usimamizi wa miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inayofadhiliwa na wadau wa maendeleo.