Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo (Ijumaa, Septemba 2, 2016) amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) na Ujenzi wa Kituo cha Tiba cha Kimataifa cha Muhimbili katika eneo la Mloganzila.

Majaliwa ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi iweke mpango maalumu wa kuongeza wataalamu zaidi katika sekta ya afya ndani ya nchi ili kuipunguzia Serikali gharama za kusomesha wataalam hao nje ya nchi.

Amesema Serikali zilizotangulia zimefanya kazi kubwa na nchi imefikia hatua nzuri ya kuongeza wataalam ndani ya nchi ambao watakwenda kutatua changamoto ya upungufu wa madaktari bingwa kwenye hospitali za mikoa na wilaya.

Pia amesema ujenzi wa kituo hicho cha tiba cha kimataifa pia utawapunguzia wananchi adha ya kutafuta fedha za kwenda kupata matibabu nje ya nchi. Tayari upasuaji mkubwa wa magonjwa ya moyo umeanza kufanyika nchini.

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Bw. Humphrey Polepole awasake watu wote waliohusika na wizi wa lita 1,000 za mafuta ya kuendeshea mitambo katika karakana ya mkandarasi anayejenga Kampasi hiyo.

“Wafanyakazi waache wizi. Lita 1,000 zinaondokaje katika karakana ya mkandarasi? Hii kampuni inayolinda kama imeshindwa kazi iondolewe na Mkuu wa wilaya usimhurumie mwizi,” amesisitiza.

Huku Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema kukamilika kwa kampasi ya Mloganzila kutasaidia upatikanaji wa madaktari bingwa wengi nchini ambao watapunguza gharama za kupeleka wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Ephata Kaaya alisema kukamilika kwa hospitali pamoja na kampasi yote ya chuo kutawezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa wataalamu wa afya nchini.

Amesema hospitali hiyo itatumika kutoa huduma za afya za kitaalam zaidi kwa magonjwa mbalimbali, hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu. Pia itapunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Ujenzi wa mradi huo umegharimu Dola za Kimarekani milioni 61, ambapo Serikali imetoa Dola milioni 18 na Serikali ya Korea imetoa mkopo wa Dola milioni 43. Kukamilika kwa ujenzi wa kampasi hiyo ya Mloganzila kutawezesha  chuo kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa fani ya afya kutoka 4,010 hadi 15,000.

Prof.  Kaaya amesema mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo ulisainiwa tarehe 12, Desemba, 2014 na ujenzi ulianza mwezi Julai, 2015 na unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2016.

Picha: Majaliwa atembelea Muhas- Mloganzila
Makamu Wa Rais Afrika Kusini Azindua Kondom Zenye Ladha Bungeni,Wapinzani Wamzomea