Mshambuliaji kutoka nchini Sweden, Zlatan Ibrahimovic, amethibitisha ataondoka jijini Paris mwishoni mwa msimu huu, na kujiunga na klabu nyingine yoyote huku klabu za England zikipewa nafasi ya kumnasa.

Ibrahimovic, amethibitisha taarifa za kuondoka kwake, mara baada ya mchezo wa jana wa ligi ya nchini Ufaransa ambapo ilishuhudia PSG wakichomoza na ushindi wa mabao tisa kwa sifuri dhidi ya Troyes, huku mshambuliaji huyo akifunga mabao manne.

Akifanyiwa mahojiano na baadhi ya waandishi waliokua wamehudhuria katika mchezo huo, Ibrahimovic alisema iwe isiwe ni lazima ataondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu, ili akasake mahala pengine ambapo patampa changamoto ya kupambana.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34, alienda mbali zaidi kwa kutoa mfano ambao unadhihirisha hatosalia klabuni hapo kwa msimu ujao, ambao katu hauwezi kutokea kwa gharama yoyote.

Alisema atakubali kubaki PSG, endapo mnara wa jijini Paris (Eiffel Tower) utabadilishwa na kuweka sanamu yake ndipo atakapokua tayai kubadili mawazo.

Hata hivyo alipoulizwa mwenyekiti wa klabu ya PSG, Nasser Al Khelaifi kuhusu kuondoka kwa Zlatan, alisema bado wana nafasi ya kukutana na mchezaji huyo na kuzungumzia mustakabali wake, huku akionyesha kuwa na imani watafanikiwa kumbakisha.

Zlatan, anatarajia kumaliza mkataba wa kuitumikia PSG mwishoni mwa msimu huu, na tayari klabu za Manchester United na Arsenal zote za England, zimeshaanza kutajwa kumuwania.

Costa Kutumikia Adhabu Kwa Mchezo Mmoja
Video: Wamarekani watumia Wimbo wa Kendrick Lamar Kumpinga Donald Trump