Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ‘TPLB’ kwa kushirikiana na Tv3 chini ya Startimes Media, wameingia makubaliano ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya michezo ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara ‘Championship’ kwa michezo iliyobaki.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam, Afisa Habari wa Bodi hiyo, Karim Boimanda alisema makubaliano ni kurusha mechi bure kutangaza ligi ili ipate thamani na kutoa fursa kwa wadhamini wengine kuiunga mkono msimu ujao.

“Ligi ya Championship nchini imekuwa ni miongoni mwa ligi zenye mvuto katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa sababu ina wachezaji wengi wa ndani na nje ya nchi ambao wanaleta ushindani kama ilivyo Ligi Kuu isipokuwa changamoto iliyopo hawakuwa na mdhamini kwa hiyo tunakaribisha wadhamini waje warushe bure kuipa thamani,” alisema.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Tv3, Ramadhan Msemo alisema fursa hii ya kuonesha ligi itawasaidia wachezaji na timu kujitangaza na kujiuza na hivyo kuongeza mapato ya klabu au wachezaji kununuliwa na klabu nyingine na mifuko yao kujaa.

Simba SC: Tunaenda kusaka heshima Morocco
Serikali yazindua mradi wa ghala uhifadhi mazao ya Chakula