Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa amekanusha taarifa kuwa endapo wapinzani watapewa nafasi ya kuingia ikulu nchi haitatawalika.

Lowassa ambaye leo anatajiwa kujua fomu ya kugombea urais kwenye ofisi za Makao Makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alikanusha taarifa hizo jana wakati akiongea katika makao makuu ya Chama Cha Wananchi CUF yaliyoko Buguruni, Dar es Salaam na kuwataka wananchi kuzipuuza taarifa hizo.

“Wameanza kuwatisha wafanya biashara, wanawatumia TRA, wahindi wanawambia Ukawa wakiingia madarakani nchi haitatawalika. Nataka kuwaambia waongo wakubwa, nchi itatawalika. Ukawa ikiingia madarakani nchi itatulia tuliii,” alisema.

Mgombea huyo wa Ukawa ambaye alienda katika ofisi hizo kuwasalimia wanachama wa CUF na kuwatia moyo kufuatia kujizulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wao wa muda mrefu, Profesa Ibrahim Lipumba, aliwataka wanachama hao kuendeleza umoja wao kwa kuwa umoja huo ndio tiketi ya kushika dola.

Alisema endapo vyama vya upinzani havitaitumia fursa hiyo adimu mwaka huu itakuwa vigumu kwa wao kushika dola hadi miaka 50 ijayo.

Katika hatua nyingine, Lowassa aliukosoa uchumi wa serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete. Alisema tangu awamu ya nne ilipoingia madarakani thamani ya shilingi ya Tanzania ilishuka mara mbili dhidi ya dola ya Marekani.

Aliwahoji wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula mbalimbali ikiwemo mchele, ambapo wananchi waliitikia kuwa umepanda mara mbili baada ya utawala wa serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na Benjamini Mkapa.

“Kwa miaka 50 Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alizungumzia kuhusu umaskini hadi leo bado tunazungumzia suala la umasikini, maradhi na ujinga kwanini? Kwa nini tunakubali kuendelea kuwa nyuma. Inabidi tufike mahali tujiuleze kwanini Waganda, Wakenya, Wanyarwanda watupite kwa uchumi,” alisema Lowassa.

 

Profesa Lipumba Awajibu Ukawa, Asema Wamejichanganya
Benteke Atangaza Uadui Na Tim Sherwood