Zikiwa zimebaki siku tano tu kuifikia Oktoba 25, siku ambayo watanzania wanatarajiwa kuweka historia mpya ya kuichagua Serikali ya Awamu ya Tano kupitia uchaguzi wenye ushindani zaidi katika historia ya vyama vingi nchini, viongozi wa vyama vya siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wameendelea kutoa kauli zinazokinzana.

Akiwa Mbeya mjini, jana mgombea urais kupitia Chadema anayeungwa mkono na vyama vya upinzani, Edward Lowassa amesisitiza kauli ya kulinda kura iliyotolewa na mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, kauli ambayo inakinzana na ile ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi inayowataka wananchi kurudi majumbani kwao mara tu baada ya kupiga kura.

Mbowe aliwataka wafuasi wa chama hicho wenye uwezo wa kubaki katika eneo la kupigia kura, wahesabu hatua 200 ambazo ni sawa na mita 200 kisha waweke ‘kambi’ katika eneo hilo, akidai kuwa umbali huo ni halali kisheria.

Edward Lowassa akihutubia maelfu ya wakazi wa Mbeya Mjini

Edward Lowassa akihutubia maelfu ya wakazi wa Mbeya Mjini

Ukinzani wa kauli za viongozi wa Chadema na muongozo uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi umeendelea kuzua sintofahamu kati ya wananchi, hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa onyo kali kwa wote watakaokaidi muongozo huo wa Tume.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Chadema alilalamikia mfumo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa bado sio huru licha ya kuomba ifanyiwe marekebisho kwa muda mrefu.

“Kwa zaidi ya miaka 25 ya vyama vingi, tumepiga kelele tukidai Tume mpya na Tume huru ya uchaguzi, kilio chetu hiki hakikusikika. Kwa sababu wenzetu kwenye Chama Cha Mapinduzi waliamini kwamba tukiwa na Tume huru ya Uchaguzi, uwezekano wa CCM kubaki madarakani haupo,” alisema Mbowe na kudai kuwa hadi sasa Tume ya Uchaguzi sio huru.

Lowassa alipata mapokezi makubwa Mbeya Mjini, mapokezi ambayo yanadaiwa kuwa yalivunja rekodi ya mikutano yote ya kampeni ikiwa na pamoja na mikutano aliyowahi kuifanya awali katika eneo hilo.

Wijnaldum Awachekesha Waliokua Wamenuna
Magufuli Kuwezesha Tafiti Kuinua Uchumi