Rais wa Marekani, Barack Obama amerusha kombora jingine dhidi ya mgombea wa Republican, Donald Trump ikiwa ni siku chache baada ya kumalizika kwa mdahalo wa pili wa wagombea urais wa nchi hiyo.

Obama amewataka viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho kinachomdhamini Trump kuchukua hatua mapema kuondoa udhamini wao badala ya kusikika wakidai hawamuungi mkono kwenye majukwaa.

Viongozi wengi wa Republican wiki hii wametangaza kujiondoa katika orodha ya wanaomuunga mkono Trump hasa baada ya Trump kuonekana kwenye mkanda wa video akijisifu kwa unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake.

Akihutubia katika mkutano wa kampeni wa kumpigia debe Hillary Clinton, Obama alihoji uamuzi wa viongozi wa ngazi za juu wa Republican kudai hawamuungi tena mkono mgombea huyo huku wakiwa kimya kivitendo.

“Ukweli ni kwamba, tuna watu ambao wanasema: ‘tunapinga kwa nguvu, hatukubaliani naye… lakini bado tunamdhamini,” alisema Obama. “Bado wanadhani anapaswa kuwa Rais, hiyo haiingii akilini,” aliongeza.

Ingawa wafuasi wa Trump walikuwa wakiingilia hotuba yake mara kadhaa wakipaza sauti kupinga anachosema, Obama alionekana akiwa ametulia na kupongeza hatua hiyo, “Hii ni demokrasia ikiwa inatendeka. Hii ni nzuri.”

Wafuasi wa Trump wakiingilia hotuba ya Obama

Wafuasi wa Trump wakiingilia hotuba ya Obama

Clinton ameendelea kumtesa Trump ambaye ameachwa hata na watu wake wa karibu huku akiwaita wasaliti. Hadi sasa Clinton anapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda uchaguzi wa Marekani huku akiwa amemshinda mpinzani wake huyo katika midahalo yote miwili.

Baraka The Prince ang'aka tena, Stan Bakora ajibu
Video: Makonda ataja mradi mwingine wa Bil. 8.8