Taarifa kutoka jijini Arusha zimeeleza kuwa hali ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema  (Chadema) ni mbaya baada ya kugoma kula tangu juzi akiwa mahabusu, akishinikiza kupelekwa mahakamani.

Mbunge huyo alikamatwa juzi nyumbani kwake kwa tuhuma za uchochezi, lakini Mwanasheria wake, John Mallya pamoja na Mstahiki Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro wameeleza kuwa mbunge huyo amegoma kula akidai kuwa polisi walimkamata kwa kumdhalilisha mbele ya watoto wake na kwamba hatagusa chakula hadi apelekwe mahakamani.

Kufuatia hatua hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo ameeleza kuwa kitendo anachokifanya mbunge huyo kugoma kula chakula ni kosa la jinai sawa na kujinyonga au kujiua kwa sumu.

Kamanda Mkombo amemshauri Mbunge huyo kula chakula kwani ni haki yake na kwamba leo (Jumatatu) atafikishwa mahakamani kwani hakuna mahakama inayofanya kazi Jumamosi na Jumapili.

Mwanasheria wa mbunge huyo, John Mallya ameeleza kuwa sheria inataka mtuhumiwa anapokamatwa afikishwe mahakamani ndani ya masaa 24 na kwamba endapo Polisi hawatamfikisha Mahakamani leo, wataandika barua kwenda Mahakama Kuu ili itoe agizo afikishwe mahakamani.

“Tunatoa muda, kama asipofikishwa mahakamani kesho (leo) tunaandika barua mahakama Kuu,” Mallya anakaririwa.

Lema amekamatwa wakati ambapo alikuwa akiendelea kuhamasisha maandamano na mikutano nchi nzima kupitia operesheni ya chama chake iliyopewa jina la UKUTA, waliyoipanga kufanyika Septemba 1 mwaka huu.

Kiwiko Champonza Sergio Aguero, Kujadiliwa Na Kamati Ya Nidhamu
CCM wamsifu Lowassa, Lissu naye anena