Kila inapofika tarehe 1 Disemba kila mwaka huadhimishwa siku ya UKIMWI duniani ili kueneza ufahamu wa ugonjwa wa UKIMWI.

UKIMWI ni nini?

UKIMWI ni “Upungufu wa Kinga Mwilini”, ambao hutokea baada ya mfumo wa kinga wa mtu kuharibiwa na Virusi Vya Ukimwi.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kufikia mwaka 2014 ugonjwa huu umeua watu milioni 39, Zaidi ni wanaoishi barani Afrika upande wa kusini kwa jangwa la Sahara. Kwa mwaka 2015 pekee wamefariki watu milioni 1.2 na kati yao watoto ni wengi.

UKIMWI hadi hivi sasa hauna chanjo wala tiba, lakini watu wanaweza kuuepuka ugonjwa huu kwa kuachana na ngono zembe kwa kuepuka kuchangia vifaa au vitu vyenye ncha kali.

Ukimwi unasababishwa na VVU. Kama virusi vyote, VVU vinaingia katika mwili kwa kusudi la kuzaa. Virusi haviwezi kuzaa peke yake: vinahitaji seli vinapoweza kuingia ndani yake na kutumia mfumo wa seli kwa kunakili DNA yake.

Mwanzoni, baada ya kuambukizwa, mtu anaweza kukumbwa na kipindi kifupi cha maradhi ya aina ya mafua. Kwa kawaida, hali hii hufuatwa na kipindi kirefu kisicho na dalili. Ugonjwa huu huendelea kutatiza kingamwili jinsi unavyozidi, hivyo kumfanya mtu kuwa katika hatari zaidi ya kupata maambukizi, ikiwa ni pamoja na maambukizi nyemelezi, na kansa ambayo kwa kawaida hayawaathiri watu walio na kingamwili njema.

Ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) hufasiliwa kwa msingi wa kiwango cha seli za CD4 + cha chini ya seli 200 au kutokea kwa magonjwa maalumu yanayohusiana na maambukizi ya VVU. Bila matibabu maalum, takriban nusu ya watu walioambukizwa VVU hupata UKIMWI katika muda wa miaka 10.

Watu walio na UKIMWI wako katika hatari kuu zaidi ya kupata saratani nyingi zinazosababishwa na virusi, isitoshe, watu hao mara nyingi huwa na dalili za kimfumo, kama vile homa ya muda mrefu, jasho (hasa usiku), tezi za limfu zilizofura, ubaridi, udhaifu na kupoteza uzito. Kuharisha ni dalili nyingine inayotokea katika takriban 90% ya watu wenye UKIMWI.

Kwa nini Maadhimisho kila mwaka? 

Serikali na pia maafisa wa afya huadhimisha siku hii, mara nyingi kwa hotuba au vikao kuhusu mada ya UKIMWI. Tangu mwaka 1995, Rais wa Marekani alipotoa tangazo rasmi juu ya Siku ya UKIMWI Duniani. Serikali za mataifa mengine zimefuata mtindo huu na kutoa matangazo maalum. 

UKIMWI umeua zaidi ya watu milioni 25 kati ya 1981 na 2007, na wastani wa watu milioni 33.3 wanaishi na VVU duniani kote kutoka 2009, pamoja na 2.6 milioni kuambukizwa kila mwaka, na 1.8 milioni kufa kwa Ukimwi na kuufanya kuwa moja ya magonjwa haribifu zaidi katika historia iliyoandikwa. 

Licha ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya matibabu na madawa ya kurefusha maisha katika maeneo mengi ya dunia, UKIMWI ulisababisha vifo vya watu wanaokadiriwa milioni 2 mwaka 2007, na miongoni mwao 270.000 walikuwa watoto.

Siku ya Ukimwi Duniani ilibuniwa mnamo Agosti 1987 na James W. Bunn na Thomas Netter, maafisa wawili wa habari kwa umma kwa ajili ya Mpango wa Kimataifa juu ya UKIMWI katika Shirika la Afya Duniani mjini Geneva, Uswisi. Bunn na Netter walichukua wazo lao kwa Dokta Jonathan Mann, Mkurugenzi wa Mpango wa Kimataifa juu ya UKIMWI ambao sasa unajulikana kama UNAIDS. Dr Mann alipenda wazo lao, akaliridhia na kukubaliana na pendekezo kuwa adhimisho la kwanza la Siku ya Ukimwi Duniani iwe tarehe 1 Desemba 1988. 

Ungano wa mpango wa Umoja wa Mataifa juu ya UKIMWI UNAIDS ulianzishwa mwaka 1996, na ukasimamia mipango na uendelezaji wa Siku ya Ukimwi Duniani. Badala ya kuzingatia siku moja, UNAIDS iliumba Kampeni ya Ukimwi Duniani mwaka 1997 kwa lengo la kueneza mawasiliano, kuzuia na kuelimisha mwaka mzima. 

Nchini Tanzania hali ya UKIMWI ikoje?

Rais wa taifa hilo Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia Mkutano wa Ngazi ya juu wa Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI amesema Tanzania inaunga mkono mshikamano wa kimataifa wa kutokomeza Ukimwi duniani,

tumepiga hatua kubwa tangu mgonjwa wa kwanza wa UKIMWI. VIfo vihusianavyo na UKIMWI vimepungua kwa asilimia 61 tangu maambukzi yashike kasi mwaka 2004. Tangu mkutano wa ngazi ya juu wa mwaka 2016, mataifa kadhaa yamefikia malengo yaliyowekwa ya kuchagiza hatua za kutokomeza UKIMWI, hivyo lazma tutambue mafanikio haya.” Rais Samia

Ukimwi siyo tena hukumu ya kifo nchini Tanzania kama ilivyokuwa miaka 38 iliyopita. Vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kutoka elfu 64 kwa mwaka 2010 hadi elfu 32 mwaka 2020. Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2020.”

November 14,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuelekea maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Desemba 1, 2021 alisema Serikali imepiga hatua katika kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa mujibu wa upimaji wa hiari wa Maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) umeongezeka nchini kutoka asilimia 61 mwaka 2016 hadi asilimia 83 mwaka 2019.

Alisema katika kuelekea kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru nchi imepiga hatua kubwa pia katika kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa wastani wa asilimia 50 kutoka watu 64000 mwaka 2010 hadi watu 32000 mwaka 2020.

Aliongeza kwa upande wa kiwango cha kufubaza VVU kwa wanaotumia waathirika wanaotumia ARV kimeongezeka kutoka asilimia 87 mwaka 2016 hadi asilimia 92 mwaka 2019 huku matumizi ya dawa hizo kwa waathirika pia yakiongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2016 hadi 98 mwaka 2019.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko ameishukuru Serikali kwa kuendelea kupambana na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI ili kuhakikisha jamii inakuwa salama na kuendelea kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

Naye Mwenyekiti wa Baaza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Bi Leticia Kapela ameishukuru Serikali kwa kuwajali wanaoishi na virusi vya Ukimwi hususan katika kuleta chanjo ya Uviko 19 ambayo ni muhimu zaidi kwao.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutujali sisi watu tunaoishi na virusi vya UKIMWI na sisi Baraza tutahakikisha tunashirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI,” amesema Bi Letia

Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI kwa mwaka huu 2021 yanafanyika kitaifa Jijini Mbeya kuanzia Novemba 24 hadi Disemba 1, 2021 katika Uwanja wa Luanda Nzovwe ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Mkoa wa Mbeya ambao una kiwango cha juu kabisa cha maambukizi ya VVU ni kati ya mikoa yenye kiwango kidogo (asilimia 31) cha ufahamu sahihi wa VVU/UKIMWI.

Hali ikoje kwa sasa Duniani?

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maswala ya UKIMWI, bado jukumu la kuhakikiha UKIMWI unatokomea duniani ni la watu wote na ndipo linatoa msisitizo wa “Zingatia Usawa Tokomeza Ukimwi. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko” ambayo ndiyo kauli mbiu ya siku ya UKIMWI kwa mwaka huu wa 2021.

UNAIDS inasema kwamba bila kuzingatia usawa kwa sasa kila hatua inayochukuliwa inaelekea kwenye kupigana vita na mlipuko wa kirusi kipya cha Corona na kusahau janga la muda mrefu la UKIMWI

UNAIDS inasisitiza kuwa kwa miaka 40 tangu agundulike mgonjwa wa UKIMWI wa kwanza duniani bado ugonjwa huo ni tatizo kubwa na linahatarisha kila hatua ya Maisha ya mwanadamu ikiwemo afya na uchumi wa dunia nzima.

Kila hatua zinatakiwa kuchukuliwa kuhakikisha lengo la kutokomeeza UKIMWI kwa mwaka 2030 linafanikiwa.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Disemba 1, 2021
Biteko:Wachimbaji jikingeni na Ukimwi